1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wanne wauawa katika mashambulizi ya leo Kiev

15 Machi 2022

Idadi ya watu waliokufa kutokana na mashambulizi yaliyofanyika usiku wa kuamkia Jumanne na mapema Jumanne asubuhi katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev imefikia wanne. 

https://p.dw.com/p/48WCU
Ukraine Kiew | Verletzte nach Angriffen
Picha: Felipe Dana/AP Photo/picture alliance

Meya wa mji wa Kiev, Vitali Klitschko ameyaeleza hayo na kuongeza kusema kuwa timu ya uokozi bado inaendelea kuuzima moto kuanzia mapema Jumanne asubuhi. Amesema siku ya leo imekuwa ngumu na hatari kwani mji wa Kiev ni moyo wa Ukraine na utalindwa.

Marufuku ya kutoka nje usiku

"Kwa kuzingatia uamuzi wa amri ya kijeshi kuanzia leo Machi 15 saa nne usiku tutaweka marufuku ya kutoka nje usiku mjini Kiev. Unaweza tu kwenda nje kutafuta makaazi. Marufuku itafanya kazi hadi sasa moja asubuhi ya Machi 17. Hivyo, nawataka wakaazi wote wa Kiev kujiandaa kutokana na ukweli kwamba watalazimika kubakia nyumbani kwa siku mbili," alifafanua Klitschko.

Katibu wa Baraza la Usalama la Urusi, Nikolai Patrushev amesema operesheni ya kijeshi nchini Ukraine inaenda kama ilivyopangwa. Patrushev pia amedai washauri wa Marekani nchini Ukraine wamekuwa wakiisaidia nchi hiyo kutengeneza silaha za kemikali.

Ukraine | Kriegsgeschehen in Mariupol,
Majengo katika mji wa Mariupol yakiwa yameshambuliwaPicha: Azov Battalion/AP/picture alliance

Takribani magari 2,000 ya raia yamefanikiwa kuondoka Jumanne kwenye mji uliozingirwa wa kusini mashariki mwa Ukraine wa Mariupol kupitia njia za kiutu za kuwaondoa raia. Maafisa wa baraza la jiji hilo wamesema kuwa magari mengine 2,000 yanasubiri kuondoka kwenye mji huo.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua idadi ya watu waliokuwemo ndani ya magari hayo. Magari mengine 160 yaliondoka Jumatatu. Mashambulizi makali ya Urusi yamesababisha wakaazi 400,000 kukosa maji salama ya bomba pamoja na machine za kuleta joto ndani ya nyumba. Pia yamesababisha uhaba wa chakula. Zaidi ya wakaazi 2,100 wameuawa kwenye mji huo tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24.

Hali bado mbaya Mariupol

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, imesema hali kwenye mji wa Mariupol bado ni mbaya na kwamba haikuweza kupeleka misaada kwenye mji huo. Kwa mujibu wa ICRC, maelfu ya watu bado wanateseka.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, limesema watu milioni tatu wameikimbia Ukraine, tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo, huku nusu ya hao wakiwa watoto. IOM imesema Jumanne katika takwimu za hivi karibuni, takribani mtoto mmoja anakuwa mkimbizi kila sekunde.

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF, James Elder amesema kwa wastani kila siku katika siku 20 zilizopita nchini Ukraine, zaidi ya watoto 700,000 wamekuwa wakimbizi.

Elder anasema hiyo ni sawa na kila dakika 55, akisisitiza kwamba mgogoro huu katika suala la kasi na kiwango haujawahi kushuhudiwa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Frankreich | EU Gipfel in Versailles | Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Aidha, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema Jumanne kuwa njia zote za kidiplomasia zinapaswa kuwa wazi wakati ambapo Ulaya inajaribu kuumaliza mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

Scholz amewaambia hayo waandishi habari baada ya kukutana na Mfalme Abdullah wa Jordan mjini Berlin. Amesema ni suala la kutumia njia zote za mazungumzo na kuyadumisha na kushinikiza kusitishwa kwa mapigano mara moja.

Kansela huyo wa Ujerumani pia ameipongeza hatua ya viongozi wa Poland, Jamhuri ya Czech na Slovenia kiuzuru Ukraine. Mawaziri wakuu wa nchi hizo wanakwenda Kiev Jumanne kama wawakilishi wa Umoja wa Ulaya kukutana na Rais Volodymyr Zelensky na Waziri Mkuu Denys Shmyhal. Pia mfuko wa msaada wa Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuwasilishwa kwa Ukraine.

 

(DPA, AP, AFP, Reuters)