Watu watatu wauwawa Burundi
15 Februari 2016Waziri wa usalama anayatembelea maeneo yalioshambuliwa anatarajiwa kutoa kauli ya serikali ya kufuatia hali hiyo.
Kwa mujibu mashuhuda na mwandishi kutoka shirika la habari la SOS medias nchini Burundi, maguruneti matatu yalivurumishwa na watu waliokuwa katika pikipiki katikati ya Bujumbura, wakati miripuko mingine miwili iliripotiwa kutokea katika viunga vya upande kaskazini wa jiji hilo.
Kifo cha mtoto mdogo
Mtoto mdogo ameuwawa kwa mujibu wa SOS medias, ambao walitoa picha inayodaiwa ya mtoto ya mwathirika, maiti ya mtoto imelazwa mtaani ikiwa imefunikwa kwa blanketi. Kutokea kwa miripuko ya maguluneti limekuwa kama jambo la kawaida katika jiji hilo, lakini haikuweza kufahamika mapema nani amefanya masambulizi hayo ambayo yamekuwa ya kiongezeka katika kipindi cha wiki mbili sasa.
Vikosi vya usalama, waasi na upande wa upanzani wote wanalaumiwa kwa kwa mauwaji. Msemaji wa ofisi ya rais Willy Nyamitwe alithibitisha matukio hayo kwa kusema "kama kawaida..magaidi wanawauwa raia kwa maguruneti."
Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo zaidi
Katika hatua nyingine mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanajiandaa kuiwekea vikwazo zaidi vya kiuchumi Burundi kufuatia mashambulizi yanayoendelea sasa ambayo yamesababisha zaidi ya watu 400 kufariki dunia.
Katika taarifa ya mawaziri hao vikwazo hivyo vitawalenga wale wote wenye kusababisha vurugu na ukandamizaji vyenye kufanya ukiukwaji mkubwa kabisa wa haki za binaadamu. Taarifa hiyo iliyotolewa wakati wa mkutano wao mjini Brussels, imeongeza kuwa wale wote wanaokuwa kikwazo cha suluhu ya kisiasa watalengwa.
Mwaka uliopita Umoja wa Ulaya ulizuia mali na kuweka marufuku ya kusafiri kwa maafisa wanne waliokaribu na Nkurunziza kwa kutumia nguvu kubwa katika makabiliano kwenye uchaguzi uliomrejesha madarakani kiongozi huyo.
Burundi ilitumbukia katika mgogoro mwezi Aprili, pale ambapo Rais Pierre Nkurunziza aliposhiriki na kushinda katika kinyanganyiro cha awamu ya tatu tata ya uchaguzi, jambo lililozusha maandamano, jaribio la mapinduzi lililoshindwa , mauwaji ya kila siku na uasi unaochipukia.
Mamia ya watu wameuwawa katika machafuko hayo na wengine zaidi ya 230,000 wamelikimbia taifa hilo. Shuhuda mmoja ambae hakutaja jina lake litajwe katika vyombo vya habari alisikika akisema"Hatujui kinachoendelea.lakini ni wazi wanataka kutujengea hofu. Nimesikia sauti za maguruneti matatu, na ni hapo karibu na mzunguko wa barabara, kuna watu kadhaa wamejeruhiwa."
Kiongozi wa mapinduzi yaliyoshindwa ya Mei 2015, jenerali wa zamani Godefroid Nyombare, kwa hivi sasa anadaiwa kuongoza kundi la waasi , Forebu. Waasi wameunda jeshi kwa kile wanachosema ni "kuulinda umma" wakisisitiza juu ya kuheshimiwa kwa mkataba wa amani wa la Arusha uliofungua njia ya kumalizika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe 1993-2006. Wapinzani wanasema mkataba huo umekiukwa na Nkurunziza baada ya kujiongezea muhula wa tatu.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman