1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Watu wawili wauawa Kyiv kufuatia mashambulizi ya Urusi

11 Agosti 2024

Watu wawili wameuawa akiwemo mvulana wa miaka minne katika mashambulizi ya makombora ya Urusi katika eneo la Kyiv usiku wa kuamkia leo.

https://p.dw.com/p/4jLbt
Ukraine Region Kiew | Zerstörung nach russischem Drohnenangriff
Wazima moto wakifanya kazi kwenye jengo la makaazi lililoharibiwa wakati wa shambulio la droni za Urusi mjini Kyiv. Picha: Press service of the State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Miili ya mwanamume wa miaka 35 na mwanawe wa kiume imepatikana chini ya vifusi kufuatia shambulio la makombora katika wilaya ya Brovary, eneo la Kyiv. Watu wengine watatu wamejeruhiwa pia katika shambulio hilo.

Mkuu wa utawala wa kijesi katika mji mkuu wa Kyiv Serhii Popko amesema ni mara ya pili kwa mji huo kulengwa.

Soma pia: Urusi yatuma vifaru kusini kukabiliana na Ukraine

Wakati huo huo, gavana wa jimbo la Kursk nchini Urusi amesema watu 13 wamejeruhiwa baada ya kombora la Ukraine lililodunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi hiyo kuanguka kwenye jengo la makaazi ya watu.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imefanikiwa kuzidungua droni 35 katika miji ya Kursk, Voronezh, Belgorod, Bryansk na Oryol.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha kwa mara ya kwanza kuwa jeshi la nchi hiyo limefanya mashambulizi ndani ya ardhi ya Urusi katika eneo la mpakani la Kurski, magharibi mwa Urusi.