1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Annalena Baerbock akutana na Lavrov mjini Moscow

Josephat Charo
18 Januari 2022

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock anakutana leo na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov mjini Moscow. Baerbock anafanya ziara yake ya kwanza mjini Moscow tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

https://p.dw.com/p/45g8G
Russland Moskau | Pressekonferenz Außenministerin Annalena Baerbock und Sergej Lawrow
Picha: SNA/imago images

Mkutano wake na Lavrov, ambaye ni waziri wa mambo ya nje aliyehudumu kwa muda mrefu barani Ulaya unaonekana hapa Ujerumani kama ubatizo wa moto. Baerbock anakutana na Lavrov wakati mahusiano kati ya Urusi na Ujerumani yakiwa katika kiwango cha chini kutokana na mkururu wa mizozo. Mahakama ya Ujerumani ilimtia hatiani raia wa Urusi mnamo Agosti mwaka 2019 kwa mauaji ya raia wa Georgia katika bustani moja la mjini Berlin na Ujerumani ikaituhumu Urusi kwa ugaidi unaofanywa na dola. Nchi hizo mbili zikafukuziana wanadiplomasia.

Ujerumani imeituhumu na kuibebesha dhamana Urusi kwa udukuzi wa bunge la Ujerumani mnamo mwaka 2015 na kwa shambulizi dhidi ya mwanasiasa wa upinzani Alexei Navalny kwa kutumia kemikali ya sumu aina ya Novichok. Kwa upande wake Urusi imekasirishwa na hatua ya Ujerumani kuzuwia vipindi vya lugha ya Kijerumani vinavyopeperushwa na televisheni ya taifa la Urusi ya RT.

Kabla mkutano wake na Lavrov, Baerbock, mwanasiasa wa chama cha Kijani cha hapa Ujerumani, amesema kama serikali wanataka kuwa na mahusiano imara na thabiti na Urusi. Hata hivyo amesisitiza kwamba orodha ya migogoro baina ya nchi hizo mbili ni ndefu, ukiwemo mzozo kuhusu bomba la gesi la Nord Stream 2 katika bahari ya Baltic, suala la ukandamizaji wa haki za binadamu, kuandamwa kwa wapinzani na kukwama kwa mdahalo wa Petersburg.

Russland Moskau | Außenministerin Annalena Baerbock trifft Sergej Lawrow
Baerbock na waziri Sergei LavrovPicha: Maxim Shemetov/REUTERS

Muda mfupi kabla ziara ya Baerbock wizara ya nje ya Urusi ilionya dhidi ya kurefusha mchakato wa utoaji wa leseni ya kukamilisha ujenzi wa bomba hilo la gesi.

Lavrov amehudumu kama waziri wa nje wa Urusi kwa miaka 18 na kumfanya kuwa mwanadiplomasia mwenye uzoefu mkubwa Ulaya. Kabla ziara ya Baerbock wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imemueleza Baerbock kama mdau muhimu katika ngazi ya kimataifa. Hata hivyo Urusi imeelezea kuvunjwa moyo na hali ya sasa ya mahusiano kati yake na Ujerumani, ikisema Ujerumani inajaribu kushawishi mchakato wa siasa za Urusi na propanga dhidi ya Urusi zinafanywa katika vyombo vya habari vya Ujerumani.

Baerbock anaitembelea Moscow akitokea mjini Kiev, Ukraine ambako jana Jumatatu alikutana na rais wa nchi hiyo, Volodymyr Zelensky, na waziri wa mashauri ya kigeni Dmytro Kuleba. Wakati wa ziara yake hiyo Baerbock alielezea diploamsia kama njia pekee muafaka ya kuutanzua mzozo kuhusu mpaka wa Urusi na Ukraine, ambako maelfu ya wanajeshi wa Urusi wamewekwa.

Baerbock mwenye umri wa miaka 41 aliihakikishia Ukraine msaada wa kidiplomasia katika kuutafutia ufumbuzi mzozo wake na Urusi. Alisema Ujerumani iko tayari kufanya mdahalo wa maana na Urusi, lakini akapinga wazo la kupeleka silaha Kiev.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amesema mazungumzo ya Baerbock mjini Moscow sio muendelezo wa mazungumzo ya mjini Kiev, akidokeza kwamba jitihada za kupunguza mzozo huo zitaendelea katika mifumo mingine.