1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Makame Mbarawa atetea makubaliano na DP World

14 Julai 2023

Waziri wa ujenzi na uchukuzi wa Tanzania Profesa Makame Mbarawa ametetea hatua ya serikali kuingia makubaliano ya ushirkiano na kampuni ya DP World akitaja uwezo mkubwa wa kampuni hiyo kuwezesha bandari kote duniani.

https://p.dw.com/p/4Ttam
Tansanias Minister für Bau und Verkehr, Prof. Makame Mbarawa
Picha: Eric Boniphace/DW

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa ametaja sababu za serikali kuanzisha majadiliano na kampuni ya DP World, kuwa ni pamoja na uwezo wake mkubwa katika uwezeshaji wa shughuli za bandari barani Afrika, Asia Ulaya, Amerika ya Kaskazini, lakini pia ile ya kusini na Australia.

Hii na mara ya kwanza kwa serikali kujitokeza kwa wahariri wakati sakata la mkataba huo likiendelea kuwa mada moto inayojadiliwa kila uchao.

Soma pia: Viongozi Tanzania wadai kutishiwa kuhusu suala la Bandari

Waziri Mbarawa aliyeambata na watendaji wake, ametumia jukwaa hilo kubainisha utashi wa serikali akisema hakuna ajenda yoyote iliyofichwa ambayo imewekwa kwenye mkataba huo.

Tansania | Hafen in Dar es Salaam
Bandari ya Dar es Salaam wakati ilipofanyia ukarabati. Mjadala unazidi kuwa mkali kuhusu makubaliano yalioingiwa kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP World juu ya uendeshaji wa bandari hiyo.Picha: Xinhua/picture alliance

Amesema mkataba umezingatia maslahi ya taifa na kwamba mazungumzo ya pande zote mbili yaani mwekezaji na serikali yamefanyika kwa kuzingatia sheria na matakwa ya nchi.

DP World ina uwezo uliothibitishwa

Amewakosoa wale aliowaita wapotoshaji wa mambo akisema shabaha ya serikali ni kuhakikisha sekta ya bandari inayotajwa kuzorota inaimarika na kwenda na wakati.

Hoja ya uwezekano wa bandari zote za Tanzania kumilikishwa kwa mwekezaji mmoja pamoja na suala la ulinzi na usalama maeneo ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele, serikali amesema maeneo hayo yamezingatia maslahi ya taifa.

Soma pia: Wanasheria Tanzania wajitosa sakata la ukodishaji wa bandari

Mwekezaji huyo DP World anadaiwa kupewa asilimia 8 ya maneo yote ya bandari nchini huku bandari kama Mtwara na Kigoma zikiendelea kusalia katika hali yake ya kawaida.

Waziri Mbarawa amesema  DP World ina uwezo na utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka maeneo ambapo bidhaa zinatoka hadi kwa walaji wa bidhaaa hizo.

Tansanias Minister für Bau und Verkehr, Prof. Makame Mbarawa
Waziri wa ujenzi wa uchukuzi wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wadau na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salam.Picha: Eric Boniphace/DW

Mjadala kuhusu uwekezaji huo bado ni suala linaloendelea kupewa kipaumbele katika mijadala  mingi nchini huku makundi yenye mirengo inayokinzana yakizidi kuonyesha ukosoaji wao hadharani.

Sikiliza: 

Spika wa bunge Tanzania awaonya waandishi juu ya ripoti za uwongo

Wakosoaji wake wanasema mkataba huo umeingiwa katika mazingira yaliyogubikwa na vitendo vya rushwa, ingawa hata hivyo hakuna ushahidi wowote uliowekwa hadharani.

Baadhi ya wanaharakati na wanasheria wamekwenda mahakamani kuupinga mkataba huo na wanasiasa wa upinzani wameligeuza kuwa ajenda kuu ya kisiasa kwa sasa.