Waziri Mkuu wa Congo kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye
25 Januari 2021Wabunge wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo watapiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Sylvestre Ilunga Ilunkamba ambaye anatoka chama cha rais wa zamani Joseph Kabila. Hatua hiyo imeashiria juhudi za Rais Felix Tshisekedi kujikwamua kutoka chini ya ushawishi wa Kabila.
Sylvestre Ilunga anatakiwa kujieleza bungeni kuhusu uongozi wake. Hatua hiyo inatokana na wabunge zaidi ya mia tatu miongoni mwa 500 kusaini pendekezo la kura ya kutokuwa na imani naye. Wabunge hao wengi wao ni kutoka chama cha FCC cha Kabila na ambao wiki iliyopita walikihama chama hicho na kujiunga na Rais Tshisekedi katika vuguvugu jipya la kisiasa la ''Union Sacrée''.
''Tunatumia nguvu na sheria itafuata baadae''
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanahisi kwamba rais Tshisekedi amejitanulia nafasi yake ya uongozi kufuatia juhudi za hivi sasa za kuiangusha serikali ya Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga. Delphin Kapaya ni mchambuzi wa siasa za Kongo.
''Kumuondoa Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga ni moja wapo ya mipango ya Rais Tshisekedi katika sera zake na ni katika mbinu zake za kutaka kumalizana kisiasa na ushawishi wa mtangulizi wake Joseph Kabila.''
Hata hivyo, utaratibu unaotumiwa hivi sasa na rais Tshisekedi pamoja na chama chake katika kujikwamua kutoka kwenye ushawishi wa mtangulizi wake Joseph Kabila, unakosolewa na wengi kwamba unakiuka katiba na kununi za bunge.
''Mambo haya ambayo yanafanyika bila kufuata sheria,inakuwa ni juhudi za kusema tunatumia nguvu , na sheria itakuja itafuata baadae.Na hapa sheria inafuatana na mawazo na ombi la mtu mwenye madaraka'' alisema Delphin Kapaya.
Ipi hatma ya wabunge wa FCC ?
Jumapili, chama cha UDPS cha rais Tshisekedi kilitangaza kwamba zaidi ya wabunge 300 wameunga mkono vuguvugu jipya la Union Sacrée lililoanzishwa na Tshisekedi mwezi Desemba.
Ofisi ya Waziri Mkuu imesema leo kwamba Sylvestre Ilunga yuko mjini Lubumbashi ambako ametarajiwa kukutana na Kabila ambaye ni kiongozi wa chama chake cha FCC.
Katiba ya Kongo inaelezea kwamba mbunge hawezi kukiama chama chake katikati ya muhula, na ikiwa atafanya hivyo anapoteza nafasi yake ya ubunge. Lakini katika uamuzi wa kushangaza wiki iliyopita, Mahakama ya Katiba ilielezea kwamba muhula wa mbunge hautakiwi kulazimishwa na chama chake bali mbunge anachukuwa uamuzi kwa hiari yake mwenyewe.