Waziri mkuu wa Ethiopia aahidi mageuzi
2 Aprili 2018Muungano unaotawala nchi hiyo ulimteua Abiye wiki iliyopita kuchukua nafasi ya Hailemariam Desalegn , ambaye alijiuzulu ili kusafisha njia kwa ajili ya mageuzi nchini Ethiopia , nchi ya pili yenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika na moja kati ya nchi zenye uchumi unaokua kwa haraka.
Baada ya kuapishwa , Luteni Jenerali huyo wa zamani wa jeshi alizungumzia kuhusu maridhiano na upinzani lakini hakutaja uwezekano wa kuondoa amri ya hali ya hatari iliyodumu kwa muda wa miezi sita iliyowekwa Februari mwaka huu baada ya mtangulizi wake kujiuzulu.
"Leo ni siku ya kihistoria. Tunashuhudia mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani. Leo hali yetu inatuwekea bayana fursa na vitisho," Abiye aliwaambia wabunge katika hotuba ya dakika 40 iliyotangzwa moja kwa moja katika televisheni.
"Demokrasia haiwezi kuwepo kunapokuwa hakuna haki,iwe haki za kiraia ama kiuchumi. Sisi wote tunahitaji jukwaa la kutoa sauti zetu kwa matatizo yetu," aliuambia mkusanyiko huo, ambako baadhi ya wapinzani pia waliruhusiwa kuhudhuria.
Jimbo la Oromiya , ambalo linazunguka mji mkuu Addis Ababa , limekumbwa na ghasia tangu mwaka 2015, kwa kiasi kikubwa zikichochewa na hisia za kutengwa kisiasa na kiuchumi miongoni mwa vijana wake.
Waoromo ni karibu theluthi moja ya Waethiopia wote nchini humo wanaofikia idadi ya watu milioni 100.
Maandamano
Chama tawala nchini Ethiopia cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kimekuwa madarakani tangu mwaka 1991 , wakati kilipochukua madaraka kutoka kwa utawala wa kijeshi wa Derg.
Maandamano na hali ya kutokuwa na utulivu katika jimbo la Oromiya vimesababisha kitisho kikubwa kuendelea kutawala chama hicho, na hali hiyo imeongeza wasi wasi wa kikabila.
"Tuna historia ndefu kama nchi. Lakini leo, uhusiano baina ya makundi ya kikabila umeharibika," alisema Seid Yimer , mwanasiasa kutoka katika kabila la Oromo.
"Hilo ni lazima liwe kipaumbe kwake. Anapaswa kuleta uhusiano mwema. Anapaswa kuvunja sheria ambazo zinachochea tofauti," alisema, akimaanisha mfumo wa Ethiopia wa majimbo ambao uliunda upya mipaka ya majimbo kwa misingi ya kikabila wakati ilipotekelezwa mwaka 1991.
Katika hotuba yake Abiye alizungumzia haja ya umoja wa kikabila.
Wabunge kutoka Oromiya , kabila kubwa nchini Ethiopia kwa eneo la idadi ya watu , walikaribisha uteuzi wa kiongozi kutoka katika kabila hilo kubwa ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likilalamikia kutengwa.
"Ni mara ya kwanza katika historia ya Ethiopia kwamba Muoromo amekuwa kiongozi wa nchi hiyo. Hii ni muhimu sana kwasababu Waoromo ni wengi," alisema mbunge huyo Abera Buno.
Makundi ya haki za binadamu yanasema majeshi ya usalama yamewauwa mamia ya watu na kuwafunga mamia kwa maelfu katika miaka mitatu iliyopita.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Caro Robi