1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Iceland ajiuzulu

5 Aprili 2016

Waziri Mkuu wa Iceland Sigmundur David Gunnlaugsson amejiuzulu kufuatia shinikizo lililotokana na kuhusishwa kwake na kashfa ya ukwepaji kodi, iliyofichuliwa katika kampuni moja ya kisheria nchini Panama Mossack Fonseca

https://p.dw.com/p/1IPqW
Island Premier Sigmundur David Gunnlaugsson in Reykjavik
Picha: Getty Images/AFP/H. Kolbeins

Kabla ya kiongozi huyo kujiuzulu, mamia ya watu walikuwa wameandamana mbele ya ofisi yake, kumtaka waziri mkuu huyo kuondoka.

Awali Jumanne Gunnlaugsson alipendekeza bunge la nchi hiyo livunjwe - pendekezo lilokataliwa na Rais Olafur Ragnar Grimsson. Gunnlaugsson alitoa pendekezo hilo baada ya upinzani kutaka kufanyike kura ya imani itakayopima kuwepo ama kutokuwepo kwa imani na serikali miongoni mwa wananchi.

Polisi wamekadiria mkusanyiko wa watu walioandamana ulikuwa mkubwa zaidi ya ule wa mwaka 2009, ambapo raia waliandamana huku vyombo vya kupikia kuonyesha kutoridhishwa kwao na utendaji wa maafisa wa serikali.

"Imani ya raia na serikali yao imepotea" amesema Kristjan Guy Burges, Katibu Mkuu wa chama cha Icelandic Social Democrats.

"Kilichotokea jana, hakikuwahi kutokea kabla, idadi kubwa ya watu walijitokeza kuandamana katikati ya mji, zaidi ya wale walioandamana mwaka 2009," amesema Burges na kuongeza, "Watu wanajiuliza iwapo serikali ilijifunza lolote kutokana na maandamano hayo yaliyopita, ama serikali ndi ileile na wanaiendesha serikali kama walivokuwa wakifanya kabla ya maandamano ya mwaka 2009."

Nyaraka zilizofichuliwa zilizopewa jina la Panama Papers zinaonesha kwamba waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 41 pamoja na mke wake wanamiliki kampuni kisiri nje ya nchi chini ya jina la Wintris Inc. Kampuni ambayo inadaiwa kuwa na kiasi cha dola milioni 4.2 katika benki tatu tofauti za Iceland zilizofilisika za Lansbanki, Glitnir na Kaupthing. kampuni hiyo imedhihirishwa kuwa ilifunguliwa mwaka 2007 na Gunnlaugsson pamoja na mke mtarajiwa kwa wakati huwo Anna Sigurlaug Palsdottir.

Gunnlaugsson akana kuhusika na kampuni hiyo

Island Proteste gegen Premierminister Gunnlaugson
Raia wa Iceland wakiandamana dhidi ya Waziri Mkuu GunnlaugssonPicha: Reuters/S. Johannsson

Lakini Gunnlaugsson amEsema aliuza nusu ya hisa zake katika kampuni hiyo kwa Palsdottir kwa dola moja Disemba 1, 2009 siku moja kabla ya sheria mpya ya Iceland kuanza kutekelezwa ambayo ingemtaka kutangaza rasmi umiliki wake wa kampuni hiyo, hali ambayo ingechukuliwa kama mgongano wa maslahi kwa upande wake.

Ukwepaji wa kodi ni suala nyeti nchini Iceland, nchi ambayo kwa muongo mzima uliopita ilikabiliana na mgogoro wa aina yake pale viongozi wa ngazi za juu wa benki za nchi hiyo walipogunduliwa kuhusika na udanganyifu wa kusafirisha fedha nchi za nje kwa lengo la kukwepa kodi. Baada ya kuteuliwa kama Waziri Mkuu wa nchi mwaka 2013, Gunnlaugsson aliahidi kuleta mabadiliko.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Daniel Gakuba