Waziri mkuu wa India ziarani Afrika
24 Mei 2011Manmohan Sighn anawasili jioni hii nchini Ethiopia, kituo chake cha kwanza ambako atahutubia mkutano wa kilele kati ya India na Afrika mjini Addis Ababa ambako anatazamiwa kuupigia upatu uhusiano wa kihistoria na kitamaduni kati ya bara hilo na India.I ndia ambayo ni taifa la tatu kubwa kiuchumi barani Asia imepitwa na China kiumaarufu katika bara hilo la Afrika na lengo la ziara ya waziri mkuu huyo ni kujaribu kupata nafasi ya kutambulika kama ilivyo China. Akizungumza kabla ya kuondoka India, waziri mkuu huyo alisema kwamba uhusiano kati ya India na Afrika unabakia kuwa chini ya misingi ya kujenga elimu na kubadilishana ujuzi, biashara na maendeleo katika sekta ya miundo mbinu. Bara la Afrika linaelekea katika ukuaji mpya duniani wakati India iko njiani kujiendeleza kwa kasi zaidi, kiuchumi.
India kwa upande wake inajaribu kutafuta ushawishi zaidi barani humo pamoja na uungwaji mkono katika harakati zake za kutafuta kiti cha kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataiafa, wakati baraza hilo litakapofanya mageuzi yanayolenga kuzijumuisha nchi zinazoinukia kiuchumi na zile zinazoendelea. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya India, waziri mkuu Sighn anatarajiwa kutoa mkopo wa takriban dolla millioni 600 kwa nchi hizo za kiafrika, kama hatua ya kuzionyesha nchi hizo ni kwa kiasi gani nchi yake inaunga mkono maendeleo ya Afrika ikijilinganisha na China. Makampuni ya mafuta ya serikali ya India yameanza kuwekeza katika Nigeria na Kenya, wakati China imemimina mabillioni ya Dolla katika utajiri wa Mafuta wa Sudan, Zimbabwe iliyo na utajiri wa Madini na katika sekta ya uchimbaji migodi nchini Zambia. Baada ya kuhutubia bunge la Ethiopia, akiwa pamoja na mwenzake, Meles Zenawi, na kufanya mazungumzo waziri mkuu, Singh ataelekea Tanzania kwa ajili ya mazungumzo na rais Jakaya Mrisho Kikwete katika ikulu yake jijini Dar es Salaam.
Mwandishi Saumu Mwasimba/RTRE
Mhariri Othaman Miraji.