1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Malaysia ajiuzulu

16 Agosti 2021

Waziri Mkuu wa Malaysia Muhyiddin Yassin amejizulu leo baada ya kupoteza wingi wa uungwaji mkono bungeni lakini anatarajiwa kusalia kama kiongozi wa mpito hadi waziri mkuu mwingine atakapopatikana.

https://p.dw.com/p/3z3UM
Malaysia Kuala Lumpur | Premierminister Muhyiddin Yassin
Picha: Vincent Thian/AP/picture alliance

Kuondoka kwa Muhyddin mamlakani kunajiri baada ya miezi 17 tu ofisini uamuzi ambao unaitumbukiza nchi hiyo katika mzozo mpya wa kisiasa wakati inapambana na mlipuko mkubwa wa janga la corona.

Kipindi cha utawala uliojaa ghasia cha Muhyiddin kilimalizika baada ya washirika kuacha kumuunga mkono, na anakuwa Waziri Mkuu aliyehudumu kwa muda mfupi zaidi katika historia ya Malaysia. soma Mtafaruku wa kisiasa Malaysia, Mahathir ajiuzulu

Akitangaza kujiuzulu kwake moja kwa moja kupitia runinga, Muhyiddin ametetea rekodi yake na kuwashutumu wapinzani kujaribu kutumia janga la corona ili kuchukua madaraka.

Muhyddin atahudumu kama waziri mkuu wa mpito

Malaysia Kuala Lumpur | Demonstranten fordern Rücktritt von Premierminister Muhyiddin Yassin
Viongozi wa upinzani wa Malaysia wakishikilia bango lenye ujumbe wa kumshinikiza Muhyddin ajiuzuluPicha: FL Wong/AP/picture alliance

Katika hotuba ya kujiuzulu kwake Muhyddin amesema "Kwa hivyo, leo, najiuzulu kama Waziri Mkuu na pia Baraza langu lote la Mawaziri kama inavyotakiwa na Katiba ya Shirikisho. Na natumai serikali mpya ambayo inachukua usimamizi wa nchi hii itawajali ninyi nyote, kwa sababu ndio kitu pekee ambacho ninajali. Na nitajali wakati wote, siku zote. "

Muhyiddin ambaye sasa ni waziri mkuu wa muda amedai kwamba majaribio yake ya kushughulikia janga hilo na wakati huo huo kutaka kubaki ofisini hayakufanikiwa kwa sababu ya watu ambao walikuwa na tamaa ya kunyakua madaraka, badala ya kutanguliza maisha ya watu wa Malaysia. soma Mahathir Mohamad ataka kuiongoza tena Malaysia

Kiongozi wa upinzani Anwar Ibrahim amekaribisha tangazo la kujiuzulu kwa Muhyddin kwa kusema hatua hio itaandaa njia kwa mabadiliko.

Malaysia Proteste Corona-Politik Lockdown
Picha: FL Wong/AP/picture alliance

Uchaguzi mpya 

Mfalme Sultan Abdullah amesema Muhyiddin anastahili kushikilia nafasi ya Waziri Mkuu, kwasababu ni vigumu kuandaa uchaguzi wa bunge wakati wa janga la Corona na ni uamuzi bora kwa kuzingatia ustawi na usalama wa watu.

Uchaguzi wa Malaysia unastahili kuandaliwa kufikia Mei 2023, lakini Muhyiddin wiki iliyopita alisema wangeweza kuandaa uchaguzi wa mapema kufikia Julai mwaka ujao.

Muhyiddin aliingia madarakani mnamo Machi mwaka jana bila kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu baada ya muungano uliokumbwa na kashfa kufuatia kuanguka kwa serikali ya mageuzi ya miaka miwili iliyoongozwa na  kigogo wa kisiasa katika miaka ya tisini Mahathir Mohamad.

Muhyddin alitarajiwa kupigiwa kuwa ya imani bungeni mwezi ujao baada ya kuwa chini ya shinikizo la kujiuzulu kutokana na jinsi anavyoshughulikia janga la Corona, kutokana na rekodi ya juu ya vifo na wengine wengi kulazwa hospitalini licha ya kuwekwa vizuizi kwa shughuli za kawaida nchini humo kwa miezi mitatu ili kudhibiti janga hilo.

Kuporomoka kwa serikali yake kunaongeza kipindi cha mvutano wa kisiasa kwa taifa hilo lenye watu milioni 32.

 

Vyanzo:AFP/dpa