1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Uingereza ziarani Norway na Estonia

16 Desemba 2024

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer anaitembelea Norway leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/4oAuk
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.Picha: Simon Dawson/Avalon/Photoshot/picture alliance

Anakwenda kufanya mashauriano ya kuandaa mkataba wa nishati safi kwa mazingira kati ya nchi hizo mbili kabla ya baadaye kuelekea Estonia kwa mkutano wa masuala ya usalama.

Starmer atasafiri hadi kwenye kituo cha mpakani cha kukusanya gesi ya Kaboni ambako atakutana na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store. Wawili hao watajadili mkataba wa pamoja wa masuala ya mazingira ambao watazamia kuutia saini mwanzoni mwa mwaka ujao.

Kisha viongozi hao watasafiri pamoja kuelekea mji mkuu wa Estonia, Tallinn kushiriki mkutano wa mfangamano wa kijeshi wa mataifa kadhaa ya Ulaya unaofahamika kwa kifupi kama JEF

Muungano huo ulioundwa mwaka 2014 unazijumuisha, Uingereza, Norway, Latvia, Sweden, Denmark, Iceland, Finland, Uholanzi na Lithuania. Mkutano wa mjini Tallinn utajadili mabadiliko ya hali ya usalama barani Ulaya katikati ya kitisho cha kutanuka vita vya Ukraine vilivyotokana na uvamizi wa Urusi.