1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Uturuki kulihutubia taifa baadaye leo

Josephat Charo30 Aprili 2007

Waziri mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan anatarajiwa kulihutubia taifa baadaye leo huku kukiwa na mzozo wa kisiasa kuhusu uchaguzi war ais ambao umesababisha tofauti kati ya jeshi la Uturuki na serikali iliyo na misingi ya dini ya kiislamu.

https://p.dw.com/p/CHFE
Waziri mkuu Erdogan kushoto na mgombea urais Abdullah Gül
Waziri mkuu Erdogan kushoto na mgombea urais Abdullah GülPicha: AP

Masoko ya fedha nchini Uturuki yameporomoka kibiashara hii leo huku wawekezaji wakihofia hali ya wasiwasi iliyosababishwa na hatua ya mahakama kutilia shaka harakati za uchaguzi wa rais na kufanyika kwa maandamano makubwa dhidi ya chama tawala cha AK mjini Istanbul hapo jana. Sarafu ya lira imeshuka kwa asilimia nne na dira ya bei za hisa mjini Instanbul imeporomoka kwa asilimia nane.

Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anakabiliwa na mbinyo mkubwa kutoka kwa Waturuki wasioelemea katika siasa za kidini, likiwemo pia jeshi la Uturuki. Erdogan anashinikizwa amuondoe mgombea urais wa chama cha AK, waziri wa mashauri ya kigeni, Abdullah Gul. Gul alikuwa zamani muislamu wenye itikadi kali za dini ya kiislamu na mke wake huvaa hijabu. Abdullah Gul alisema jana kwamba ataendelea kugombea katika uchaguzi huo wa rais nchini Uturuki ambao kisheria utafanywa na bunge lililo na idadi kubwa ya wabunge wa chama tawala cha AK.

´Harakati bado zinaendelea. Hii ina maana sitajiondoa katika kuwania urais; kwa sababu kushiriki kwangu sio matokeo yanayotangazwa baada ya usiku mmoja, bali itachukua muda wa mashauriano. Lazima sasa tusubiri uamuzi wa mahakama ya katiba. Hadi hapo watu wanatakiwa wawe watulivu.´

Mahakama ya katiba nchini Uturuki imeanza hii leo kuchunguza ombi la upinzani kutaka uchaguzi wa rais nchini humo uahirishwe. Hatua hii huenda isababishe uchaguzi wa bunge kufanyika mapema na wachambuzi kwa maoni yao wanasema itasaidia kuzuia machafuko kutokea nchini Uturuki.

Mahakama ya katiba nchini Uturuki imesema itajaribu kutoa uamuzi wake kufikia keshokutwa Jumatano, wakati bunge litakapokuwa likijiandaa kufanya duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Serikali ya chama cha AK, ambayo imekuwa ikiendeleza mpango wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii, unaolenga kuielekeza Uturuki kwa Umoja wa Ulaya, inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi tangu ilipochaguliwa mnamo mwaka wa 2002.

Jana Waturuki takriban milioni moja walifanya maandamano ya kuipinga serikali katika mji wa kibiashara na mkubwa zaidi nchini Uturuki, Instanbul. Waandamanaji wengi waliishutumu serikali kwa kuwa na mpango wa kuanzisha taifa la kiislamu na kuikosoa kwa kushindwa kushauriana na upinzani kuhusu uchaguzi wa rais, ambaye ana mamlaka ya kura ya turufu na mamlaka makubwa ya kuteua viongozi. Mwanamke huyu alikuwa miongoni mwa waaandamanaji mjini Istanbul.

´Tumeona kwamba maisha yetu ya baadaye yamo hatarini hasa sera ya Atatürk ya serikali kutoelemea sana dini. Ndio maana tuko hapa.´

Waturuki wasioikumbatia dini wanahofu Erdogan na Gul wanataka kuvuruga hali nchini Uturuki ambapo dini na taifa vimebakia kuwa mbali na badala yake kuileta dini karibu na taifa. Lakini waziri mkuu Erdogan amekanusha madai hayo akisema hakuna njama yoyote na kuongeza kwamba anataka kulegeza baadhi ya hatua za Uturuki kuubana uhuru wa dini.

Wafanyabiashara nchini Uturuki wamezikaribisha sera za chama tawala cha AK ambazo zimepunguza mfumuko wa bei na kuufufua uchumi baada ya miaka kadhaa ya mzozo mkubwa wa kiuchumi. Lakini sasa wafanyabiashara hao wanaunga mkono miito ya upinzani unaotaka uchaguzi mkuu ufanyike mapema nchini humo.

Hata hivyo katika hotuba yake baadaye leo waziri Erdogan hatataka kuonyesha kwamba serikali yake imeshindwa kufuatia mbinyo wa jeshi na upinzani.