1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaItaly

Silvio Berlusconi afariki dunia

12 Juni 2023

Waziri mkuu wa zamani wa Italia Silvio Berlusconi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86. Kifo cha Berlusconi kimetangazwa na msemaji wake hii leo.

https://p.dw.com/p/4SSj5
Silvio Berlusconi Nachruf
Picha: Cecilia Fabiano/LaPresse via ZUMA Press/picture-alliance/dpa

Kiongozi huyo tajiri na maarufu alilazwa katika hospitali ya Milan siku ya Ijumaa ili kufanyiwa vipimo zaidi kuhusiana na ugonjwa uliyokuwa ukimsumbua wa saratani ya damu.

Berlusconi alikabiliwa na matatizo ya afya kwa miaka kadhaa

Berlusconi aliyekuwa na ushawishi mkubwa, alikabiliwa na matatizo ya kiafya kwa miaka kadhaa, huku akifanyiwa upasuaji wa moyo mnamo mwaka 2016 na kulazwa hospitalini mwaka 2020 baada ya kupata maambukizi ya UVIKO19. Licha ya kuchaguliwa tena kuwa Seneta mwaka jana, alionekana kwa nadra hadharani.

Berlusconi aliiongoza Italia kwa miaka tisa

Berlusconi aliyesalia kuwa kiongozi wa chama chake cha mrengo wa kulia cha Forza Italia, aliongoza nchi hiyo mara tatu na kwa jumla ya miaka tisa kati ya mwaka 1994 na 2011. Aliwashawishi wapiga kura kwa ahadi ya mafanikio ya kiuchumi kabla ya kufurushwa wakati mzozo wa madeni uliikumba nchi yake.