Ujerumani yaipongeza mahakama Uturuki kuwaachia wanaharakati
26 Oktoba 2017.
Sigmar alisema Berlin inafuatilia kuachiwa huru kwa raia mwingine wa Ujerumani ambaye amefungwa katika gereza jingine nchini humo kwa makosa mengine tofauti.
Mahakama ya mjini Instabul jana iliamuru wanaharakati hao wa haki za binadamu wanane, waliokuwa wamewekwa rumande, waachiwe kwa dhamana wakati kesi yao inayohusiana na ugaidi, ikisubiri maamuzi ya mahakama. Watu wawili katika kesi hiyo inayowasisha washukiwa 11 wameachiwa huru, huku mtuhumiwa wa mwisho akishikiliwa katika kizuizi kilichoko katika mji mwingine.
Watuhumiwa hao, akiwamo Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International nchini Uturuki, Idil Eser, raia wa Ujerumani Steudtner na Msweden Ali Gharavi, walikamatwa na na polisi wakati walipohudhuria warsha ya mafunzo kuhusu usalama wa mfumo wa kidijitali, mnamo Julai mwaka huu.
Kesi yao imezidisha wasiwasi kwamba utawala wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan unazidi kuwa wa kiimla.
Washitakiwa wote hao wanatuhumiwa kuandaa mapinduzi na kusaidia wanaharakati wa Kikurdi wenye mrengo wa kushoto.
Pia wanashutumiwa kushiriki katika njama ya mhubiri wa kidini aishie nchini Marekani Fethullah Gulen, ambaye serikali ya Uturuki inamtuhumu kuratibu jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa Julai mwaka jana.
Amnesty yaapa kuendelea na harakati za mapambano
Baada tu ya kuachiwa kutoka jela, mjerumani Peter Steudtner alisema, ''Tunawashukuru sana wale wote waliotupa ushirikiano, wa kisheria, wa kidiplomasia na wa kizalendo.''
Kwa upande wake Ali Gharavi alisema hivi sasa wamepata familia kubwa mpya, na kushukuru mchango wa kila upande katika kuwezesha kuachiwa kwao.
Amnesty International ilikaribisha kuachiwa huru kwa wanaharakati hao na kuapa kuendelea na harakati za kutetea haki za binadamu nchini Uturuki.
''Leo, hatimaye, tunasherehekea kuwa marafiki zetu na wenzetu wanarudi kwa wapendwa wao na watalala katika vitanda vyao kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi minne,'' amesema Katibu Mkuu wa Amnesty Salil Shetty.
Sigmar alisema uamuzi huo wa mahakama umeonyesha kuwa wito wa Ujerumani wa kutolewa kwa hukumu ya haki umesikilizwa..
Mwenyekiti wa Amnesty, Taner Kilic, ambaye aliswekwa gerezani Juni, kesi yake inasikilizwa katika mahakama tofauti akihusishwa na padri wa Marekani, Fethullah Gulen.
Kilic anatuhumiwa kuajiriwa na mtandao wa Gulen wa kutumia mfumo wa simu wa meseji za siri.
Gulen mwenyewe ameyakana mashtaka hayo ya kuongoza jaribio la kuipindua nchi.
Uturuki iliwakamata watu 50,000 tangu jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka jana na kuwafuta kazi serikalini, karibu watumishi 110,000.
Mwandishi: Florence Majani(AP)
Mhariri: Daniel Gakuba