Baerbock akutana na waziri mkuu wa Lebanon Najib Mikati
11 Januari 2024Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amekutana na Waziri mkuu wa Lebanon Najib Mikati, wakati akiendelea na ziara yake ya Mashariki ya Kati.
Mazungumzo yao huenda yalituama katika mapigano yanayoendelea baina ya kundi la wanamgambo wa Kishia wa Lebanon Hezbollah na Israel, ambao wamekuwa wakirushiana risasi za moto katika eneo la mpakani katika siku za hivi karibuni.
Ziara ya Baerbock Mashariki ya Kati: Baerbock airai Israel kuwalinda Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi
Baerbock pia atakutana na wanajeshi wanaohusika na ujumbe wa Umoja wa Mataifa UNIFIL, ambao tangu mwaka 1978 umekuwa na jukumu la kulinda amani kwenye mpaka wa Lebanon na Israel.
Ujerumani imeshiriki katika ujumbe huo tangu mwaka 2006, ikiwa na jumla ya wanajeshi 200, pamoja na meli za jeshi la wanamaji. Ziara ya Lebanon ni kituo cha mwisho cha safari ya nne ya Baerbock Mashariki ya Kati tangu Oktoba 7.