Waziri wa Ulinzi Kongo azuru eneo la machafuko Beni
28 Septemba 2020Akiwahutubia wakaazi wa Beni waliomlaki katika barabara inayotokea Mbau kwenda Kamango, kilomita zipatazo hamsini kaskazini mashariki ya Beni, waziri wa ulinzi Ngoie Mukena, ametaka usalama kuimarishwa.
Matamshi hayo ya waziri hayaambatani na hali halisi ya mambo katika eneo hili, wilaya ya Beni ikiwa kila uchao inashuhudia mauwaji ya wakaazi kwa kukatakatwa kwa mapanga na waasi kutoka Uganda ADF. Mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji wa Beni Kizito Bin Hangi amesema, kuwa wanachosubiri baada ya hotuba ya waziri wa ulinzi ni kuona ADF wanatokomezwa, na watu hawauawi tena.
Soma pia: Vita visivyokwisha vya makundi ya wanamgambo nchini Congo
Ziara za viongozi wa jeshi pamoja na mawaziri mbalimbali katika mji na wilaya ya Beni katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Bunia pamoja na Djugu katika mkoa wa Ituri, zinatajwa na wakaazi wa mashariki ya Congo, kuwa hazijawahi kuzaa matunda ambayo ni amani.
Wakati waziri wa ulinzi akiwa anaandamana na mkuu wa majeshi ya Congo pamoja na wabunge wa kitaifa, wanaohusika na masuala ya ulinzi, kwakiendelea na ziara yao hapa Beni, ADF nao walikuwa wakiendelea kuwauwa watu.
Miili ya watu watano waliouawa na waasi hao iligunduliwa jana katika kijiji cha Mbutaba, katika kongamano la Batangi Mbau.
Soma pia: Wanamgambo wa CODECO waingia mji wa Bunia DRC
Baadhi ya wakaazi wametekwa nyara na waasi hao, na kupelekwa msituni, na haijulikani kama bado wako hai, au wameshauawa.
Baada ya Beni, waziri wa ulinzi pamoja na ujumbe wake, wamekwenda Goma, kabla ya kwenda Bukavu katika mkoa wa Kivu ya Kusini, na hatimae Kalemie katika mkoa wa Tanganyika, kutathmini hali ya usalama mdogo inayojiri katika mikoa hiyo.