1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa zamani wa mambo ya nje kuwania urais Tanzania

6 Agosti 2020

Waziri wa zamani wa mambo ya nje nchini Tanzania, Benard Membe, amepitishwa na chama chake kipya cha upinzani kuwania urais kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/3gUbw
Tansania Opposition Bernard Membe und Maalim Seif Sharif Hamad
Picha: DW/E. Boniphace

Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo uliofanyika jijini Dar es Salaam hapo jana, ulimchaguwa mwanadiplomasia huyo kupeperusha bendera ya chama hicho kumkabili Rais John Magufuli, anayewania kurejea madarakani kwa muhula wa pili.

Membe alifukuzwa kwenye chama tawala cha Mapinduzi, CCM, ambacho Magufuli ni mwenyekiti wake, kwa kile anachosema ni kuonesha dhamira ya kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Kwa upande wa Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye mamlaka yake ya ndani, chama hicho kimempitisha Maalim Seif Sharif Hamad, kuwania tena nafasi ya urais, hii ikiwa ni mara ya sita kwa mwanasiasa huyo mkongwe kugombea urais wa visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi kupitia upinzani.

Tayari chama chengine kikuu cha upinzani, CHADEMA, imewatangaza wagombea wake, na wengi wanaamini kuwa vyama hivyo viwili huenda vikaunga nguvu kukikabili chama kinachotawala, CCM, ambacho kimekuwapo madarakani tangu uhuru wa nchi hiyo, takribani miongo sita sasa.