Westerwelle atiwa kishindo na FDP mpaka ajiuzulu
4 Aprili 2011Uamuzi wa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle kujiuzulu kama mwenyekiti wa chama cha kiliberali cha FDP ndio mada iliyohanikiza magazetini hii leo.Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 40 amejizulu pia wadhifa wake wa naibu kansela.
Tuanzie Bielefeld ambako gazeti la "Neue Westfälische linasema:
Anataka kuendelea lakini na wadhifa wake kama waziri wa mambo ya nchi za nje ingawa hata huko hana nafasi nzuri ya kung'ara.Nyanja muhimu za kisiasa anaziongoza mwenyewe kansela Angela Merkel.Majukumu yaliyombakia katika wizara yake,Westerwelle ameyachezea. Kujizuwia Ujerumani kupiga kura katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa ,lilikuwa kosa kubwa la kuhuzunisha alilolifanya.Westerwele anang'oka,nani atachukua nafasi yake, bado hajulikani.La muhimu zaidi lakini ni nani atachaguliwa kushika nafasi yake.Ili kuweza kusalimika,FDP wanahitaji muongozo wa aina mpya badala ya mkondo wa kiliberali wa kiuchumi.
Gazeti la "Der neue Tag" la mjini Weiden linahisi ingekuwa bora kama FDP wangewageukia wazee kwa sasa na sio vijana.Gazeti linaendelea kuandika:
Ikiwa waliberali wanataka kuranda upya uwanjani,wanabidi waachane na fikra ya kuwakabidhi vijana uongozi na badala yake waelekeze dira upande wa wazee.Mtu mwenye maarifa mfano wa mwenyekiti wa zamani wa FDP Wolfgang Gerhardt,mwenye umri wa miaka 67,si mzee hivyo kushindwa kuirejesha marekebu inayo yumba yumba katika bahari iliyo tulivu na salama.Pindi FDP wakilazimika kukalia viti vya upinzani bungeni baada ya uchaguzi wa mwaka 2013,akina Rösler na Lindner watakua bado na wakati wa kutosha kukinyanyua chama chao na kukipatia sura mpya.
Gazeti la "Nordwest-Zeitung" lina maoni kinyuma na hayo,na linaandika:
Chama cha FDP kimejipatia fursa mpya ya kuchipuka.Wakimchagua Philipp Rösler kushikilia wadhifa wa mwenyekiti, wana FDP watakuwa wamempata mwanasiasa mwenye kipaji,aliyedhihirisha ujuzi wake chamani na serikalini katika jimbo la Niedersachsen.Wakimtoa pia Rainer Brüderle na mtaalam Daniel Bahr kukabidhiwa wizara ya afya,hapo FDP watakuwa sio tuu wametoka katika kizazi kikongwe na kuingia katika kizazi kipya,bali pia wenye ujuzi watakuwa wamekabidhiwa hatamu za uongozi wa chama hicho cha kiliberali kinacho lega lega.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed