WHO: COVID-19, fedha vyakwamisha mapambano ya malaria
30 Novemba 2020Katika ripoti yake ya mwaka kuhusu ugonjwa wa malaria duniani iliyotolewa leo Jumatatu, WHO imesema maendeleo ya kupambana na ugonjwa huo yamekwama katika miaka ya hivi karibuni hasa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kuna visa vingi pamoja na vifo.
WHO imesema mwaka 2019 kulikuwa na takriban maambukizi milioni 229 ya malaria duniani, takwimu ambazo zilikuwa sawa na za miaka minne iliyopita na kwamba vifo vya malaria vinaweza kuzidi vile vitokanavyo na janga la COVID-19, huku wengi wao wakiwa watoto.
Soma zaidi: WHO: Vifo vitokanavyo na Malaria huenda vikaongezeka mwaka huu Afrika
Kwa mujibu wa shirika hilo, watu 409,000 duniani walikufa kwa ugonjwa wa malaria mwaka 2019, wengi wao wakiwa kutoka maeneo masikini ya Afrika, ikilinganishwa na watu 411,000 kwa mwaka 2018.
Kampeni za malaria ziliendelea
Hata hivyo, ripoti hiyo imegundua kuwa kampeni nyingi za kupambana na malaria ziliendelea wakati huu wa janga la virusi vya corona, lakini kuna wasiwasi kwamba juhudi za kukabiliana na malaria zinaingiliana na mzozo wa COVID-19 ambao unakwamisha juhudi hizo na kurudisha nyuma zaidi mapambano.
Mkurugenzi wa WHO anayehusika na mpango wa malaria, Pedro Alsonso, amesema kutokana na mzozo wa corona, nchi nyingi zimefunga mipaka yake na viwanda hatua ambayo pia inazuia au inakwamisha kupelekwa kwa vyandarua vya kujikinga na mbu pamoja na dawa za malaria.
Aidha, serikali zimezielekeza rasilimali zake katika kupambana na janga la COVID-19, ambazo pia zilikuwa ni gharama za kupambana na malaria.
Mkurugenzi wa WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti amesema virusi vya corona vinatishia kukwamisha juhudi za kupambana na malaria. Moeti amesema licha ya COVID-19 kuuathiri uchumi wa Afrika, washirika wa kimataifa wanahitaji kuongeza juhudi kuhakikisha kwamba rasilimali zinaongezwa katika miradi ya malaria ambayo inaleta mabadiliko.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Gebreyesus amesema ni muda kwa viongozi wa Afrika na dunia kwa ujumla kuamka tena na kupambana na malaria. WHO imesema upungufu wa fedha za kupambana na malaria unaleta kitisho kikubwa, huku ikiwa na dola bilioni 3 kati ya dola bilioni 5.6 zilizochangishwa 2019.
Zaidi ya asilimia 90 ya ugonjwa huo uko barani Afrika, ambapo watu 384,000 walikufa mwaka uliopita. Nigeria ilikuwa na asilimia 27 ya vifo hivyo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo asilimia 12, Uganda asilimia tano na Msumbiji asilimia nne.
Ripoti ya WHO imesema nchi 21 zimefanikiwa kuutokomeza ugonjwa wa malaria katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Nje ya Afrika, India imeendelea kupata faida kubwa katika miaka miwili iliyopita, huku ikipunguza asilimia 18 ya maambukizi na asilimia 20 ya vifo.
Peter Sands, Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa dunia wa kupambana na UKIMWI, kifua kikuu na malaria amesema ripoti ya WHO imetolewa kwa wakati unaofaa.
(DPA, AFP, Reuters)