1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaanza kuchunguza chimbuko la corona, China

29 Januari 2021

Wataalamu wa afya wa WHO wanaochunguza chimbuko la virusi vya corona watembelea hospitali moja mjini Wuhan nchini China ambayo ni moja kati ya hospitali za kwanza kuwatibu wagonjwa katika siku za kwanza za mripuko huo.

https://p.dw.com/p/3oZ9C
China l WHO-Experten in Wuhan beginnen mit Untersuchung
Picha: The Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Kundi hilo linaloongozwa na shirika la WHO lililotoka chini ya karantini ya wiki mbili hapo jana Alhamisi, linapanga kutembelea maabara, masoko na hospitali katika muda wake uliosalia wa wiki mbili mjini Wuhan ambapo kisa cha kwanza cha corona kiligunduliwa mwishoni mwa mwaka 2019. Mkuu wa kitengo cha dharura wa WHO Mike Ryan, amesema kuwa shirika hilo limetafuta uthibiti wa matarajio nakusema hakuna hakikisho la majibu kwa sasa. Mmoja wa wataalamu wa ujumbe huo wa WHO Thea Fischer, hapo jana aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba ni muhimu kukumbuka kuwa mafanikio ya kundi hilo na kufuatilia asili ya virusi hivyo vinategemea kikamilifu uwezo wa kufikia vyanzo husika.

Wakati huo huo, Waziri wa idara ya magereza nchini Uingereza Lucy Frazer amesema leo kuwa nchi hiyo haitachapisha mkataba wa chanjo kati yake na kampuni ya AstraZeneca kwa sababu hatua hiyo itahatarisha usalama wa kitaifa. Alipotakiwa na redio ya LBC kuelezea kwa nini serikali ina wasiwasi kuhusu kuchapishwa kwa mkataba huo, Frazer alisema kuwa pale ilipostahili umma kuarifiwa imefanyika, lakini ikiwa hali hiyo itahatarisha usalama kwa sababu yoyote basi hawastahili. Alipotakiwa kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo la usalama wa kitaifa, Frazer alisema kwamba huo ndio uelewa wake.

Coronavirus Impfstoff Symbolbid
Chanjo ya corona ya kampuni ya AstraZenecaPicha: picture-alliance/Flashpic

Huku hayo yakijiri, mzozo kati ya Umoja wa Ulaya na kampuni ya kutengezea chanjo ya AstraZeneca kuhusu kutolewa kwa chanjo uliongezeka huku kampuni hiyo ikijitetea dhidi ya madai kwamba imekiuka kujitolea kwake katika mkataba uliopo na pande hizo mbili zikagongana kuhusu mipango ya mazungumzo zaidi. Kwa mara ya kwanza, afisa mkuu wa kampuni hiyo ya AstraZeneca, Pascal Soriot alizungumzia kuhusu mvutano huo na kukanusha madai ya Umoja wa Ulaya kwamba kampuni hiyo ilikuwa inashindwa kutimiza ahadi yake ya kutoa chanjo za virusi vya corona.

Katika mahojiano na gazeti la Italia La Republica, Soriot alisema takwimu za utoaji wa chanjo hizo katika mkataba wa kampuni hiyo ya AstraZeneca na Umoja wa Ulaya zilikuwa malengo na sio thibitisho kamili na kwamba malengo hayo hayakuweza kuafikiwa kwa sababau ya matatizo ya kupanua kwa haraka uwezo wa uzalishaji.

Baada ya kuchapishwa kwa mahojiano hayo, msemaji wa Umoja wa Ulaya alisema kampuni hiyo ilijiondoa katika mazungumzo siku ya Jumatano kuhusu matatizo na utoaji wa chanjo madai yaliyokanushwa na kampuni hiyo, lakini saa chache baadaye, Umoja wa Ulaya ulisema kuwa mazungumzo yanaendelea.