1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yatahadharisha juu ya uhaba wa chanjo ya kipindupindu

21 Machi 2024

Shirika la afya duniani WHO limetahadharisha kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kukabiliana na ongezeko la ugonjwa wa kipindupindu.

https://p.dw.com/p/4dxNR
Muuguzi akitoa chanjo ya kipindupindu wakati wa kampeni ya kutoa chanjo katika hospitali ya Kuwadzana mjini Harare
Muuguzi akitoa chanjo ya kipindupindu wakati wa kampeni ya kutoa chanjo katika hospitali ya Kuwadzana mjini HararePicha: Jekesai Njikizana/AFP

Tahadhari hiyo imetolewa katika wakati ambapo dunia inakabiliwa na uhaba wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo wa kuharisha.

Shirika la kimataifa la kuratibu usambazaji wa chanjo ICG, limesema mamilioni ya watu wanakabiliwa na hatari ya kupata kipindupindu kwa sababu kampuni pekee inayozalisha chanjo dhidi ya ugonjwa huo, EuBiologics ya Korea Kusini, imelemewa na mahitaji.

Soma pia: Mripuko wa kipindupindu Kenya

Kupitia taarifa, shirika hilo limeeleza kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu duniani kote.

ICG imeongeza kuwa, uzalishaji wa chanjo duniani mwaka huu utakuwa kati ya dozi milioni 17 na milioni 50 japo idadi hiyo huenda ikawa ndogo ukilinganisha na mahitaji ya wagonjwa.

Wagonjwa wa kipindupindu waongezeka

Mgonjwa wa kipindupindu akiwa ndani ya wodi ya wagonjwa waliotengwa katika hospitali ya Bwaila mjini Lilongwe, Malawi
Mgonjwa wa kipindupindu akiwa ndani ya wodi ya wagonjwa waliotengwa katika hospitali ya Bwaila mjini Lilongwe, MalawiPicha: Thoko Chikondi/AP Photo/picture alliance

Mnamo mwaka 2022, idadi ya wagonjwa wa kipindupindu waliorodeshwa na WHO iliongezeka mara mbili kutoka mwaka 2021 hadi wagonjwa 473,000 ilhali mwaka huu, idadi hiyo imeongezeka na kufikia wagonjwa 700,000.

Ugonjwa wa kipindupindu husababisha mtu kuhara au hata kutapika na kusababisha upungufu wa maji mwilini na wakati mwengine hata kifo, iwapo mgonjwa hatatibiwa haraka.

Soma pia: UNICEF yatoa hadhari ya kusambaa Kipindupindu nchini Kongo 

Kipindupindu husababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoitwa kwa lugha ya kitaalamu "Vibrio cholerae".

Nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Haiti, Somalia, Sudan, Syria, Zambia na Zimbabwe.