Wiki ya Ukweli katika Mazungumzo ya Mabadiliko ya Tabianchi
10 Desemba 2019Wiki ya ukweli imeanza katika mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi mjini Madrid nchini Uhispania. Miito, maandamano na nasaha zilihanikiza mtindo mmoja mnamo wiki ya mwanzo ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi. Sasa kwa hivyo mawaziri wanaingilia kati mazungumzoni. Waziri wa mazingira wa serikali kuu ya Ujerumani Svenja Schulze wa kutoka chama cha SPD ni miongoni mwa wanaohudhuria. Mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg wa Sweeden anataka kuitumia fursa hiyo kuzungumza na wanasayansi kuhusu wito wake kwa wanasiasa.
Kwa Thunberg na maelfu ya wanaharakati wengine wa mazingira, waziri wa mazingira wa Ujerumani na wenzake wanaokutana mjini Madrd wana jukumu la kufafanua mipango ya kupambana na kuzidi hali ya ujoto ulimwenguni hadi ifikapo mwisho wa wiki hii."Tumebakiwa na miaka kumi tu kuweza kujiepusha na balaa" amesema Teresa Ribera mbele ya wawakilishi kutoka mataifa 200."Sote tunabidi tuwe wanaharakati ili kuepusha balaa la kuzidi hali ya ujoto duniani, amesema waziri huyo wa mazingira wa Uhispania.
Marekani inawajibika licha ya kitisho cha kujitoa katika makubaliano ya Paris
Wakati huo huo mgombea kiti cha rais nchini Marekani Michael Bloomberg anapanga kushirki katika mkutano huo wa kimataifa akidhamairia kubainisha "Marekani inaendelea na mapambano dhidi ya kuzidi hali ya ujoto duniani licha ya kitisho cha kujitoa katika makubaliano ya Paris.
Baada ya spika wa baraza la wawakilishi la Marekani bibi Nancy Pelosi wiki iliyopita, hivi sasa itakuwa zamu ya meya wa zamani wa New-York kuhutubia mkutano huo wa kimataifa.""Nnakwenda katika mkutano wa kimataifa mjini Madrid, kwasababu rais Trump hatokwenda" alisema Michael Bloomberg katika risala yake kupitia mtandao wa Twitter.
"Itasaidia kuwapa watu moyo" amesema Sébastien Treyer, ambae ni mkurugenzi wa taasisi ya maendeleo endelevu na uhusiano wa kimataifa. Ameongeza kusema "ziara ya Bloomberg inadhihirisha kuna wadau wa kiuchumi, na mashirika ya kijamii, waliopania kupambana na mabadiliko ya tabianchi."