WikiLeaks yautikisa tena ulimwengu wa kidiplomasia
29 Novemba 2010Kutoka Pakistan hadi Sweden, ulimwengu wa kidiplomasia na kijasusi unajiona umevuliwa nguo. Hata kwa ufalme wa Saudi Arabia, rafiki mkubwa wa utawala wa Marekani, safari hii mambo yako hadharani. Dunia haina shimo la kuifukia siri, ndivyo mtandao wa WikiLeaks unavyojaribu kuthibitisha. Uhuru wa kujieleza na kusambaza habari katika ulimwengu wa Magharibi sasa umeanza kuwatokea puani wenyewe.
Mwendeshaji wa mtandao huo, Julian Assange, anasema wao ni taasisi inayofahamu majukumu yake, na hata kama nchi kama Marekani zilijitahidi kuwazuía kuchapisha taarifa hizi, lakini kutokuchapisha "kungelikuwa na maana ya kutokuuanika udhalilishaji unaofanywa na taasisi husika ulimwenguni.
Nchini Pakistan, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, Abdul Basit, ameuita uchapishwaji wa taarifa hizi kama laana. Serikali yake imetajwa kwamba imekuwa ikifanya kazi kwa siri na Marekani kuyaondoa madini ya yuraniamu kwenye mitambo yake ya nyuklia kwa khofu kwamba yanaweza kuja kutumika kutengeneza silaha. Basit amekanusha taarifa hizo, akisema kwamba Pakistan ni taifa huru lenye mamlaka kamili na linalolinda maslahi yake, na hivyo lisingeliweza kufanya jambo kama hilo.
Lakini katika taarifa nyengine, WikiLeaks inasema kwamba Mfalme Abdullah wa Saudia Arabia aliiambia Marekani kwamba Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan, ndiye kikwazo katika eneo hilo, maana "kichwa kikioza, huoza mwili mzima." Japo Basit halipingi hili moja kwa moja, lakini anasema si juu yake kulizungumzia.
Israel haijaonesha kushtuka, licha ya kutajwa kuwa inashinikiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya Iran. Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa nchi hiyo ameliambia Shirika la Habari la AFP, na hapa namnukuu: "Angalau taarifa hizi zinasema kuwa sisi sio ndumilakuwili. Kile tunachokisema faraghani, ndicho hicho hicho tunachokisema hadharani. Mataifa mengi ya Kiarabu yanataka hatua za kijeshi dhidi ya Iran, lakini hayasemi wazi."
Hivyo ndivyo taarifa za WikiLeaks zinavyofichua. Kwamba mataifa ya Kiarabu, kama Saudi Arabia na Bahrain, wanaishinikiza Marekani iivamie Iran kijeshi.
Nchini Iran kwenyewe, leo hii (29 Novemba 2010) miripuko miwili ya mabomu ilimuua mwanasanyansi wa kinyuklia wa nchi hiyo, Dokta Majid Shariari, na kumjeruhi mwenzake, Dokta Fereydoon Abbasi.
Tayari, ripoti za vyombo vya habari nchini humo zimeyaunganisha mauaji hayo na taarifa za WikiLeaks. Mtandao wa televisheni ya taifa ya nchi hiyo umechapisha taarifa inayosomeka: "Katika tukio la uhalifu wa kigaidi, mawakala wa utawala wa Kizayuni wamewashambulia maprofesa wawili wa chuo kikuu walipokuwa wakienda kazini."
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Hoshyar Zebari, ameuita uchapishwaji wa taarifa hizi za WikiLeaks kama jambo lisilosaidia hata kidogo. Ameiambia AFP kwamba katika wakati ambao ndio kwanza serikali mpya ya Iraq inaanza kazi, halikuwa jambo la busara kuchapisha taarifa ambazo zinaweza kabisa kuhatarisha usalama wa nchi hiyo na raia wake.
Sweden kwenyewe, ambako ndiko anakotokea mwendeshaji wa WikiLeaks, waziri wa Mambo ya Nje, Carl Bildt, ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, kwamba taarifa hizi zinaidhoofisha diplomasia si ya Marekani tu, bali ya ulimwengu mzim, a kwa ujumla, kwani sasa mtu hajui amuamini nani katika masuala mazito ya siri za usalama na ujasusi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/DPAE
Mhariri: Othman Miraj