Wilders ashinda uchaguzi kwa kishindo Uholanzi
23 Novemba 2023Kulingana na matokeo kamili, Chama chake cha Uhuru PVV kilishinda viti 37 bungeni, zaidi ya mara mbili ya viti kilivyopata katika uchaguzi uliopita na kuwashinda wapinzani wake. Kambi ya mrengo wa kushoto ilifuatia nyuma kwa ushindi wa viti 25, huku chama cha VVD cha mrengo wa kati kikiambulia viti 24, matokeo mabaya kwa chama cha Waziri Mkuu anayemaliza muda wake Mark Rutte.
Soma pia: Waholanzi wapiga kura kumchagua waziri mkuu mpya
Wilders, mwenye umri wa miaka 60, sasa ana kibarua kigumu cha kujaribu kuunda muungano kwa kuwashawishi wapinzani ambao kimsingi walikataa kuhudumu katika serikali inayoongozwa na PVV kabla ya kupiga kura.
Ushindi huo wa kishindo ambao haukutarajiwa umeibua pongezi za haraka kutoka kwa viongozi wenzake wa mrengo mkali wa kulia nchini Ufaransa na Hungary lakini kuna uwezekano mkubwa utazua hofu mjini Brussels. Wilders anapinga Umoja wa Ulaya na anataka kupigwa kura juu ya "Nexit" ambayo ni ya kujiondoa kwenye jumuiya hiyo.
Sera ya Uhamiaji
Akiwahutubia wafuasi waliokuwa wakishangilia mjini The Hague baada ya matokeo ya uchaguzi, Wilders alisisitiza ahadi yake dhidi ya wahamiaji, akisema Waholanzi walipiga kura kukomesha kile alichokitaja kama "tsunami" ya wanaotafuta hifadhi.
"Lakini bila shaka ni kuhusu hatua unazochukua. Na Uholanzi sasa imepiga kura kwa wingi ikiwa na viti 35 kwa PVV. Sera ya uhamiaji na hifadhi inahitaji kupinduliwa kabisa. Kwamba mambo lazima yawe tofauti, kwamba mambo lazima yawe makali zaidi."
Ingawa Wilders alipunguza makali ya kuupinga Uislamu wakati wa kampeni, mpango wa chama cha PVV uliahidi kupiga marufuku Quran, misikiti na vazi la Kiisalam lahijabu, na sasa viongozi wa jumuiya ya Kiislamu nchini Uholanzi wana wasiwasi kuhusiana na ushindi huo. Muhsin Köktaş, mwenyekiti wa taasisi ya Mawasiliano kwa Waislamu na Serikali.
"Kipindi kigumu kinakuja kwa Waislamu nchini Uholanzi. Ikiwa mpango wa PVV utatekelezwa, usalama wa maisha ya Waislamu hautahakikishwa tena. Hiyo ina maana kwamba sisi kama Waislamu hatuwezi kuishi, na hatuwezi kutekeleza ibada zetu, dini yetu. Tunaamini katika demokrasia na utawala wa sheria. Watu wa Uholanzi wamechagua, na ninaheshimu hilo.vLakini kama Muislamu wa kidini na wa utendaji, nina wasiwasi. Hakika tutapita, kuhusu wasiwasi wetu, na tuendelee kuzungumza na serikali, Hatuna chaguo lingine." Alisema Köktaş.
Hata hivyo licha ya ushindi wa kishindo, haijabainika ni jinsi gani Wilders anaweza kunyakua kwa pamoja viti 76 anavyohitaji kwa wingi katika bunge lenye viti 150.
//AFP,dpa