Leverkusen yaishushia kichapo cha 4-0 Feyenoord
20 Septemba 2024Mabingwa hao wa Ujerumani walichukua uongozi katika dakika ya tano ya mchezo baada ya Wirtz kupiga mkwaju maridadi kutoka umbali wa karibu yadi 20.
Mabao mengine ya Leverkusen yalifungwa na Alex Grimaldo kabla ya mlinda lango wa Feyenoord Timon Wellenreuther kujifunga mwenyewe kunako dakika ya 45 ya mchezo.
Wirtz mwenye umri wa miaka 21 alituzwa mchezaji bora wa mechi japo ameeleza kufurahishwa na kucheza kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Soma pia: Leverkusen waufungua msimu wa Bundesliga kwa ushindi
"Bila shaka nina furaha kwa kutuzwa mchezaji bora wa mechi na pia kwa kufunga mabao mawili. Lakini kitu cha muhimu zaidi kwangu ni kwamba timu ilipata ushindi.”
"Mechi hii ilikuwa maalum kwangu, hatimaye nimecheza katika ligi hii ya mabingwa Ulaya. Natarajia kucheza mechi nyengine zaidi.”
Wakati Leverkusen iliposhiriki kwa mara ya mwisho katika hatua ya makundi yapata miaka miwili iliyopita, Wirtz alikuwa anauguza jeraha la msuli wa nyuma ya paja.
Tangu wakati huo, kiungo huyo stadi ameonyesha uwezo mkubwa uwanjani na anatajwa kuwa tunu katika soka la Ujerumani na hata barani Ulaya. Wirtz alicheza kila mechi msimu uliopita na kusaidia Bayer Leverkusen kuwa timu ya kwanza kukamilisha msimu mzima wa Bundesliga bila kupoteza hata mechi mmoja.
Soma pia: Mashabiki wa Dortmund kuandamana kupinga udhamini wa Rheinmetall
Leverkusen ilishinda taji la ligi kuu Bundesliga, Kombe la shirikisho la Ujerumani DFB-Pokal na kufika fainali ya ligi ya Ulaya Europa League.
Ulikuwa ni mchezo wa kiufundi kutoka kwa Leverkusen ambao walipiga mashuti machache kuelekea lango la mpinzani wake kuliko hata Feyenoord.
Hiki kilikuwa kipigo cha kwanza cha Feyenoord tangu Brian Priske achukua mikoba ya kuiongoza klabu hiyo ya Uholanzi akichukua nafasi ya kocha Arne Slot aliyejiunga na Liverpool msimu huu.