1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa amani watolewa katika maeneo yenye mizozo Kenya

Wakio Mbogho21 Septemba 2021

Kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani ya mwaka huu nchini Kenya, wadau mbalimbali wamehimizwa kuhakikisha kunakuwepo mazungumzo ya uwazi katika kuelewa vyanzo vya machafuko ili kujenga jamii zilizo na uthabiti, haki na usawa. Taifa hilo limeshuhudia matukio ya jamii kuzozana. Licha ya juhudi za amani matatizo yameendelea kushuhudiwa. Sikiliza ripoti ya mwandishi wetu Wakio Mbogho.

https://p.dw.com/p/40cZE

Mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel Ole Kenta, anaelezea ghadhabu yake kutokana na mizozo ya kijamii katika mpaka wa Nakuru na Narok.

Mchakato wa amani unaoendelea unaongozwa na ujumbe wa viongozi wa ngazi za juu, kwenye azimio la kusuluhisha machafuko ya mara kwa mara kuhusu rasilimali yanayoshuhudiwa kwenye eneo hilo.

Watu saba wakiwemo watoto wanne wamefariki kufuatia mapigano eneo hilo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Naibu Gavana wa Nakuru Erik Korir ni mmoja wa viongozi ambao wanakemea matamshi ya uchochezi.

Katika miezi ya hivi karibuni, jamii zilizoko Baringo, Turkana, Pokot, Isiolo, Marsabit na Laikipia zimeshiriki vikao, kujadili mikakati ya kudumisha amani baina yao. Lakini mara nyingi hali ya uhasama kati ya jamii hizi huwa haichelewi kujirudia tena.

Mchakato wa maridhiano kati ya serikali na upinzani uluioanzishwa na Rais Kenyatta na kiongozi wa Raila Odinga ulidaiwa kuleta utulivu na amani baada ya vurugu zilizokumba taifa hilo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Mchakato wa maridhiano kati ya serikali na upinzani uluioanzishwa na Rais Kenyatta na kiongozi wa Raila Odinga ulidaiwa kuleta utulivu na amani baada ya vurugu zilizokumba taifa hilo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.Picha: AFP/T. Karumba

Walter Mwania, mkereketwa wa masuala ya kiusalama kupitia mpango wa PROACT Kenya, anasema sababu kuu ni kwamba msingi wa mizozo yenyewe huwa haijatatuliwa. Jamii hizi huzozania umiliki wa ardhi, mipaka, wizi wa mifugo na uwakilishi wa kisiasa.

Kwenye maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Amani, Asha Mohammed, katibu mkuu wa shirika la Msalaba Mwekundu nchini anahimiza umuhimu wa mazungumzo ya wazi na ya kina katika kuelewa vyanzo vya mizozo.

Kuna hofu kwamba hali ya ukame inayoshuhudiwa nchini huenda ikaibua uhasama zaidi hasa kati ya jamii za wafugaji wanaotembea kuwatafutia mifugo wao lishe.

Serikali ilitangaza kwamba zaidi ya watu milioni mbili kutoka kaunti 12 wameathiriwa na janga hilo, na huenda hali ikawa mbaya zaidi iwapo kiangazi kitaendelea.  

Visa vya machafuko au mizozano ya kijamii hushuhudiwa nchini Kenya hususan katika misimu ya siasa au uchaguzi.
Visa vya machafuko au mizozano ya kijamii hushuhudiwa nchini Kenya hususan katika misimu ya siasa au uchaguzi.Picha: Reuters/B. Ratner

Akizungumzia maadhimisho ya leo kwenye hafla iliyofanyika mjini Nakuru, Francis Kooli, Balozi wa Amani, ambaye pia ni kamanda wa polisi eneo la Kisii amelaani mizozo inayochechewa kisiasa.

“Kama maafisa wanaotekeleza sheria, tunawaomba Wakenya wasiruhusu tena matumizi ya bunduki na mabomu ya kutoa machozi. Hatutaki kutumia vifaa hivi kwa sababu ya ukosekanaji wa amani. Tutumie nguvu hizo kwa ujenzi wa taifa. Tunaporuhusu amani kuharibiwa, juhudi zote za maendeleo zinaangamia. Kama tunataka kuendelea kama taifa, ni lazima tuilinde amani,” amesema Kooli.

Tume ya uwiano na utangamano nchini, NCIC, imehusika katika kuleta uwiano kwenye maeneo haya na mara nyingi imebaini kwamba wanasiasa wametumia vyanzo hivi vya uchochezi kuwagawanya watu kwa misingi ya kijamii ili wapate uungwaji mkono.

Aidha, imebainika kuwa baadhi ya kesi ambazo huwasilishwa mahakamani na makundi ya kiraia yanayojitokeza kuzisaidia jamii zilizoathirika huwa haziwakilishi maoni ya wengi wa waathiriwa.

Walter Mwania ametoa mfano wa wajamii wa Ogiek ambao sasa wanataka umiliki binafsi wa ardhi baada ya miaka mingi ya kumiliki ardhi kijumla kama jamii.