Umoja wa Ulaya wahitaji ushirikiano wa Marekani kuikoa WTO
27 Septemba 2021Mkuu wa masuala ya biashara katika umoja wa Ulaya Valdmis Dombrovski amesema Marekani inahitaji kushirikiana na Umoja wa Ulaya kuleta mageuzi katika shirika la biashara duniani WTO kuliko kuliacha shirika hilo kuzorota kwa kulitelekeza. Makamu huyo wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya ameweka wazi kwamba mageuzi yanahitajika na wala sio kuliangamiza shirika hilo. Matamshi yake ameyatowa wakati akihutubia katika chuo kikuu cha John Hopkins mwanzoni mwa wiki ya mazungumzo na wenzake wa Marekani mjini Washington.
Dombrovski amesisitiza kwamba kuliacha shirika la biashara duniani WTO liporomoke itakuwa ni kukipoteza moja ya chombo muhimu katika suala la maendeleo na biashara ya usawa. Lakini pia amesema ni suala la kuamua kati ya kufuata utaratibu wa sheria inayoeleweka au sheria ya mwenye nguvu mpishe. Marekani inaendeleza sera za rais aliyetangulia Donald Trump ya kuzuia teuzi za bozi ya maamuzi ya shirika hilo la biashashara duniani na hatua hiyo inamaanisha kwamba shirika hilo haliwezi kuwa na nguvu za kuingilia kati na kuitatua migogoro ya kibiashara duniani.
Dombrovski anasema Umoja wa Ulaya unautambua wasiwasi wa Marekani kuhusu kuwa na shirika la WTO linalofanya kazi na haja ya kushughulikiwa kwa dharura suala linalohusu tabia ya kutokuwepo usawa kama vile suala la kutolewa ruzuku kubwa kwa viwanda, ulazimishaji wa kuhamisha teknolojia, ruzuku na kujiingiza kwa kiasi kikubwa wa serikali katika masuala ya uchumi.
Shirika la WTO haliwezi kuzishughulikia changamoto hizi likiwa kama lilivyo hivi sasa kwa mujibu wa kamishna wa Umoja wa Ulaya akitilia mkazo kwamba mchakato wa mageuzi unahitajika kuanzia katika mkutano wa ngazi ya mawaziri wanachama wa shirika hilo mnamo mwezi Novemba 30 hadi Desemba 3.
Dombrovski amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kufanya kazi na Marekani kufikia makubaliana kuhusiana na ruzuku kwenye sekta ya uvuvi, afya, kilimo na maendeleo endelevu pamoja na kuanza mazungumzo ya dhati kuhusu mageuzi ya kitaasisi. Dombrovski ameongeza kuweka wazi kwamba anaamini ukiwepo ushirikiano imara na uongozi wa pamoja hapana shaka shirika hilo la WTO litapata nguvu mpya.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/rtre
Mhariri: Daniel Gakuba