1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WTO yapania biashara huru duniani

Admin.WagnerD3 Desemba 2013

Mkutano wa siku nne wa mawaziri wa biashara wa nchi wanachama wa Shirika la Biashara Duniani-WTO unaendelea katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia katika jaribio la kuifanya biashara ya dunia kuwa huria.

https://p.dw.com/p/1AST0
Picha: Reuters

Mkutano huu wa siku nne wa mawaziri ambao ni wa tisa unalenga katika kurahisisha utaratibu wa forodha, kupunguza mtindo wa serikali kufidia wakulima katika nchi tajiri na kuzipa msaada nchi masikini. Shirika la biashara duniani limetabiri kwamba makubaliano yatakayofikiwa bali yataweza kufungua nafasi mpya 21 milioni za kazi na hasa katika nchi zinazoendelea na kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji wa dola 960 bilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa WTO Roberto Azavedo.
Mkurugenzi Mkuu wa WTO Roberto Azavedo.Picha: picture-alliance/dpa

Matumaini ya kufufuliwa mazungumzo ya Doha
Pindi mkutano huu utamalizika kwa mafanikio utaweza pia kuyafufua mazungumzo yaliokwama ya Doha kuhusu kuwekwa viwango vya biashara . Washiriki wengi wanaamini pia kushindwa mkutano huu kunaweza kuhujumu zaidi umuhimu wa Shirika la biashara duniani, kuwa jukwaa la biashara la kimataifa.

Baadhi ya nchi ikiwemo India, zimevipinga baadhi ya vifungu katika kile kinachoitwa mpango wa Bali,na hivyo kuuweka mashakani uwezuekano wa kupata makubaliano. Katibu mku wa WTO Roberto Azevedo, amewataka wawakilishi wa nchi 159 wanachama kuonyesha nia na utayarifu wa kupata maridhiano.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Jumanne, Azevedo pia, alisema Mkutano huu wa mawaziri wa biashara kisiwani Bali ni nafasi pekee ya kupata maridhiano au kuyazika kabisa. Alitamka, "ama ni sasa au tusahau." ameutaja mkutano huo kuwa muhimu zaidi katika kipindi cha miaka kadhaa.

Hatari ya mikataba mbadala
Wengi hivi sasa wanaliona Shirika hilo kuwa lenye kuhatarishwa na kile kinachowezekana kuwa ni mikataba mbadala baina ya mataifa makubwa kibiashara zikiwemo nchi 12 zinazounda Jumuiya ya ushirikiano wa nchi za bahari ya Pacific-TPP, kutokana na shinikizo la Marekani.

Luz Caballero, mwakilishi wa Peru katika WTO.
Luz Caballero, mwakilishi wa Peru katika WTO.Picha: DW/M. Banchón

Waziri wa biashara wa Indonesia Gita Wirjawan -nchi mwenyeji wa mkutano- huo- amesema anamatumaini makubaliano yatafikiwa na kuwataka wajumbe kujiepusha kuwa mateka kwa sababu ya misimamo inayotafautiana ,isipokuwa watafute njia muwafaka kufikia maridhiano.

Upinzani dhidi ya WTO
Mnamo siku ya Jumanne waandamanaji wapatao 400 walidai Shirika la biashara duniani livunjwe. Maandamano hayo yalitayarishwa na mashirika ya kilimo na uvuvi yasiokuwa ya kiserikali

Mmoja wa waandalizi alisikika akisema kuwa shirika la WTO ndiyo chanzo cha njaa duniani na ukosefu wa ajira kwa wakulima wengi. Hakukuweko na ghasia zozote wakati wa maandamano hayo, lakini pamoja na hayo ulinzi ulikuwa mkali na polisi wakihakikisha waandamanaji wanabakia mbali na eneo la mkutano.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Yusuf Saumu