1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi Jinping aonya dhidi ya kuanzisha Vita vipya Baridi

Saleh Mwanamilongo
25 Januari 2021

Rais wa China ametahadharisha kuhusu kile alichokiita kuwa ni mwanzo wa vita vipya baridi na ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa dhidi ya Corona.

https://p.dw.com/p/3oOLH
China | Xi Jinpings Ansprache zum Online-Weltwirtschaftforum Davos
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/L. Xueren

Mkutano wa kila mwaka unaojulikana kama Jukwaa la Kiuchumi Duniani, umefunguliwa leo kwa njia ya video. Rais wa China Xi Jinping ndie aliyefunguwa mkutano huo huku nchi yake ikijiimarisha kiuchumi. Masuala mengine yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo ni pamoja na janga COVID-19. 

Rais wa China, Xi Jinping ametahadharisha kuhusu kile alichokiita kuwa ni mwanzo wa vita vipya baridi na ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya corona.

''Mwaka uliopita ulikumbwa ghafla na janga la COVID-19. Afya ya umma iliathirika vibaya ulimwenguni kote. Na kulishuhudiwa mdororo mkubwa wa kiuchumi duniani. Ulimwengu ulikumbwa na mizozo kadhaa ambayo ni nadra kutokea ulimwenguni.''

EU na mbinu za kurejesha ukuwaji uchumi

Ratiba ya kikao cha leo itaiangalia taswira ya uchumi wa ulimwengu, huku watunga sera wa Ulaya, wakiwemo Mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya, Christine Lagarde na mawaziri wa uchumi wa Ufaransa na Ujerumani Bruno Le Maire na Peter Altmaier, wakijadili mbinu za kurejesha ukuaji wa uchumi.

Rais wa Marekani Joe Biden hatohudhuria mkutano huo wa wiki nzima, kwa sababu anakabiliana na changamoto za dharura na ngumu nchini mwake. Biden atawakilishwa kwenye mkutano huo na mshauri wake wa masuala ya afya na janga la virusi vya corona, Anthony Fauci na John Kerry ambae ni mjumbe maalumu wa mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson (kushoto), waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson (kushoto), waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Viongozi wakubwa kutoka Ulaya watakaohudhuria ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa UIaya Ursula von der Leyen. Rais wa Urusi, Vladimir Putin atahutubia pia kwenye mkutano huo.

Nchi za Asia pia zinahudhuria mkutano huo unaojulikana kama ''Wiki ya Mjini Davos''. Mbali na rais wa China, rais wa Korea ya Kusini na Waziri Wakuu wa India na Japan pia wanahudhuria.

Shirika la Oxfam laomba kodi zaidi kwa matajiri

Kama kawaida tangu lilipoasisiwa jukwaa hili la Davos miaka 51 iliyopita, kutakuwa pia na mikutano ya faragha miongoni mwa wakuu wa makampuni ya biashara na viongozi wa serikali kuhusiana na vitega uchumi. Mada nyingine muhimu itakayojadiliwa wiki hii ni ongezeko la tofauti ambazo zinahatarisha mshikamano wa jamii ulimwenguni.

Kwenye ripoti yake ya mwaka iliyotangazwa leo Jumatatu, Shirika la kimataifa linaloendesha harakati za kupinga umaskini, Oxfam lilitoa mwito wa kuongeza kodi kwa watu na makampuni tajiri ilikupambana na ukosefu wa usawa ulimwenguni. Shirika la Oxfam linasema kuna mabilionea waliojirundikia fedha nyingi mnamo kipindi cha janga la virusi vya corona.