Watoto wakabiliwa na utapiamlo Yemen
27 Oktoba 2020Taarifa kutoka Umoja mataifa zinasema, Yemen ipo katika hali ngumu wakati huu wa janga la Corona na upungufu katika ufadhili wa msaada unazidisha mzozo wa kibinadamu.
Takwimu zinaashiria kuwa zaidi ya visa nusu milioni vya viwango vya juu utapiamlo kati ya watoto chini ya miaka mitano vimerekodiwa kusini kwa nchi hiyo huku takwimu kutoka maeneo ya kaskazini zikiendelea kuratibiwa lakini kuna matarajio kuwa hali itakuwa kama ilivyo kusini mwa Yemen
Soma zaidi:Yemen na kitisho kipya cha njaa
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya shirika la Chakula na kilimo, Shirika la mpango wa chakula na Umoja Mataifa kitengo cha kushughulikia maswala ya watoto UNICEF asilimia 15.5 ya visa hivyo vimewaacha takriban watu 98,000 katika hatari ya kufariki iwapo hawatapokea matibabu ya haraka.
"Takwimu wanazotoa zinathibitisha kuwa utapiamlo mkali miongoni mwa watoto umefikia viwango vya juu zaidi tangu kuanza kwa vita nchini humo," amesema Lise Grande, mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja Matiafa Yemen.
Janga la COVID-19 limeongeza kadhia ya Yemen
Yemen imegubikwa na vita tangu mwaka 2014, kati ya kundi la waasi wa Kihouthi linaloungwa mkono na Iran, na serikali iliyovunjika ambayo inaungwa mkono na muungano wa kijeshi Saudia na kuizamisha Yemen katika mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu.
Aidha Umoja Mataifa umedokeza kuwa kuongezeka kwa mzozo na kupungua kwa uchumi, pamoja na athari kubwa ya janga la Covid -19, kumeongeza kadhia ya Wayemen kufikia ukingoni, huku mipango ya misaada pamoja na misaada wa dharura ya chakula kuvurugika kutokana na ukosefu wa fedha.
Yemen inahitaji Dola bilioni 3.2 kukabiliana na tatizo hilo na kufikia mwezi Oktoba imepokea Dola bilioni 1.43 pekee.
Mwezi September Umoja Mataifa umesema kuwa huduma muhimu katika vituo vya afya 300 zimesitishwa na zaidi ya thuluthi tatu ya huduma zao za misaada ya kiutu zimepunguzwa au kuondolewa kabisa.
Soma zaidi:Mamia warejea nyumbani katika ubadilishaji wafungwa Yemen
Saudi Arabia na wafadhili mbali mbali kutoka mataifa ya Kiarabu, wameshindwa kutimiza ahadi zao za msaada wa kiutu wakati ambapo wanakabiliwa na chanagamoto za kiuchumi kutokana na janga la Corona.
Huku hayo yakijiri waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammed Javad Zarif ameutaka Umoja Mataifa kuchukua hatua dhidi ya msimamo wa Marekani juu ya vita vilivyotokea tangu 2001.
AFP/AP