Yuko wapi Ballack na wenzake?
7 Septemba 2012Lakini wote hao hawaichezei tena timu ya taifa na hakuna mmoja kati yao aliye na mkataba wowote na klabu kwa sababu wanaonekana ni kama hawahitajiki tena baada ya kuisha makali. Ballack, mwenye umri wa miaka 35, ndiye aliye maarufu zaidi kati ya hao wanne, baada ya mkataba wake wa miaka miwili na nusu katika klabu ya Bayer Leverkusen kumalizika Juni 30. Nyota huyo anasema atafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake katika wiki chache zijazo. Mchezaji huyo wa zamani wa Bayern Munich na Chelsea alihusishwa na uvumi wa kuhamia ligi ya soka ya Marekani, lakini hakuna lililofanyika.
Mshambuliaji wa Ujerumani na pia klabu ya Bayern Munich Mario Gomez sasa amepona jeraha na anaendelea kufanya mazoezi ya kifundo chake cha mguu wa kushoto, ikiwa ni wiki nne baada ya kufanyiwa upasuaji.
Gomez mwenye umri wa miaka 27 ambaye alimaliza msimu wa mwaka jana wa Bundesliga, kama mfungaji bora wa pili wa mabao nyuma ya Klaas-Jan Huntelaar wa Schalke, alifanyiwa upasuaji Agosti saba na anatarajiwa kuendelea kuwa mkekani kwa wiki kadhaa.
Tayari amekosa mechi mbili za kwanza za Bundesliga msimu huu na pia yuko nje ya kikosi cha Ujerumani cha mechi za kufuzu kwa kombe la dunia. Nafasi yake kwa sasa katika klabu ya Bayern imechukuliwa na Mcroatia Mario Mandzukic ambaye kufikia sasa amefunga magoli manne katika mechi tatu. Bayern wanaongoza orodha ya timu za Bundesliga baada ya mechi mbili za uzinduzi msimu huu.
Mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney, amesema hatuay yake ya kuomba uhamisho kutoka Old Trafford miaka miwili iliyopita lilikuwa kosa kubwa zaidi katika taaluma yake. Rooney ambaye aliwekwa nje ya kikosi cha Uingereza kilichocheza mchuano wa kufuzu kwa kombe la dunia dhidi ya Moldova mjini Chisinau kwa sababu ya jeraha la paja, aliyasema hayo katika kitabu chake ambacho kinachapishwa na gazeti la Daily Mirror.
Rooney alitaka kuihama klabu hiyo kwa sababu ilishindwa kutimiza matarajio yake. Hata hivyo, baada ya siku kadhaa akabadilisha wazo hilo na akatia saini mkataba mpya wa mika mitano, lakini sasa anasema analikumbuka jambo hilo kwa majuto. Miji itakayokuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia la FIFA nchini Urusi mnamo mwaka wa 2018 itatangazwa mwezi huu. Taarifa ya Kamati ya maandalizi ya Urusi imesema tangazo hilo kwa pamoja na FIFA litatolewa Sptemba 29.
Miji 13 ya Urusi – Moscow, St Petersburg, Kaliningrad, Yaroslavi, Nizhny Novgorod, Kazan, Samara, Saransk, Volgograd, Krasnodar, Rostov, Sochi na Yekaterinburg inawania kupewa haki ya kuandaa tamasha hilo kubwa ulimwenguni. Mkuu wa kamati ya maandalizi nchini humo, Vitaly Mutko, anasema kinyang'anyiro hicho kitachezwa katika viwanja 12 kwenye miji 11. Moscow ina viwanja viwili. Luzhniki ambao utaandaa fainali una viti vya washabiki 90,000
Jose Mourinho anasema Real Madrid haitataka kufanya kosa lolote katika mechi zake za kundi gumu la Ligi ya Mabingwa, na anatabiri kibarua kikali na Manchester City. Katika awamu ya makundi mabingwa hao wa La Liga watapambana na mabingwa wa Uingereza, Manchester City, mabingwa wa Bundesliga, Borussia Dortmund, na mabingwa wa Uholanzi, Ajax Amsterdam.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/DPA/AFP
Mhariri:Miraji Othman