Zaidi ya waandishi habari 57 wauwawa 2016
19 Desemba 2016Shirika hilo linalotetea uhuru wa waandishi habari limesema kwamba nchini Syria pekee ni waandishi 19 waliuwawa ikifuatiwa na Afghanistan ambako waandishi 10 walipoteza maisha, huku tisa wakiuwawa Mexico na watano Iraq.
Takribani waandishi wote waliouwawa duniani katika mwaka 2016 walikuwa ni waandishi wa ndani ya nchi walizouwawa.
Ingawa idadi ya waandishi wa habari waliouwawa mwaka huu ni ndogo ikilinganishwa na ile ya waandishi habari zaidi ya 67 waliouwawa mwaka 2015, shirika la RSF linasema sababu kubwa iliyochangia idadi ya waiouwawa kupungua ni kwamba wengi wa wanahabari wamezikimbia nchi zao, ambazo zimeendelea kuwa hatari na hasa nchi kama Iraq, Libya, Yemen Afghanistan na Burundi.
Ripoti inataja kwamba kutoroka kwa waandishi habari katika nchi hizo zenye migogoro kumechangia kuwepo kwa kiasi kikubwa pengo la utoaji habari na taarifa katika nchi hizo ambako viongozi wamejiwekea kinga za kutoshitakiwa.
Waandishi 348 wako jela
Mbali na waandishi wa vyombo vya kawaida vya habari, kunatajwa pia kwamba wanablogu tisa na wafanyakazi wanane wa vyombo habari waliuwawa ndani ya mwaka huu.
Vile vile, kufikia sasa na waandishi habari 348 wanaoshikiliwa jela.
RSF inasema sababu nyingine ya kupungua kiasi kwa vifo vya waandishi habari kumetokana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na kile kinachoitwa waangamizaji uhuru wa vyombo vya habari ambao wamekuwa mara zote katika harakati za kuvifungia vyombo vya habari pamoja na kuwatisha waandishi habari.
"Katika nchi kama Mexico hali hiyo ilisababisha waandishi habari kujiwekea utaratibu wa kuchuja taarifa wanazozitoa ili kuepuka kuuwawa", inasema ripoti hiyo ya mwaka.
Nchini Afghanistan, waandishi habari wote 10 waliouwawa walilengwa makusudi kwa sababu ya kile wanachokifanya kama waandishi, ambapo saba kati yao wakiwa wanaume na watatu wanawake, waliuwawa mwezi Januari katika mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga, ambayo kundi la Taliban lilidai kuhusika.
Mataifa hatari zaidi
Yemen, ambako zaidi ya watu 7,000 wameuwawa tangu mwaka 2015 katika vita vinavyoendelea kati ya jeshi la serikali linalosaidiwa na Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi, ni nchi nyingine iliyo hatari kwa waandishi habari ambapo waandishi habari watano wamepoteza maisha yao wakiwa kazini mwaka huu.
Katibu mkuu wa RSF, Christophe Deloire, alisema ghasia dhidi ya waandishi habari zimeendelea kushuhudiwa mwaka huu zikifanywa kwa makusudi kuwalenga waandishi. "Waandishi wamekuwa wakilengwa makusudi na kuuwawa kwa sababu tu ni waandishi," alisema katibu mkuu huyo.
Kwa mujibu wa Deloire, hali hii ya kutisha inadhihirisha kushindwa kwa juhudi za jumuiya ya kimataifa zilizolenga kuwalinda waandishi na pia "ni ishara ya kuweko dhamira dhahiri ya kuwauwa waandishi habari huru katika nchi hizo ambako imeonekana njia zote zinatumika kuchuja habari" na kueneza propaganda na hasa makundi ya siasa kali katika Mashariki ya Kati.
RSF imetoa mwito kwa Katibu Mkuu ajae wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuunda kamati yenye wajumbe maalum watakaosimamisha mpango wa kuwalinda waandishi habari duniani.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga