Zaidi ya wachimba migodi 200 wafa Uturuki
14 Mei 2014Bendera ya Uturuki ndani na nje ya nchi hiyo inapepea nusu mlingoti kuomboleza msiba huo mkubwa, huku zaidi ya watu 300 wakiendelea kukwama chini ya ardhi katika mji wa Sama ulio kwenye jimbo la Manisa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani, dpa, wakati moto uliporipuka usiku wa kuamkia leo, kwenye mgodi huo kulikuwa na watu 787. Vikosi kadhaa vya uokoaji vinashiriki kwenye uokozi na Waziri wa Nishati wa Uturuki, Taner Yiildiz, amesema hadi sasa watu waliokolewa ni 365:
"Operesheni za uokoaji zinaendelea. Hadi sasa tumeshapoteza wachimba madini wetu 201. Tunahofia kwamba idadi inaweza kuongezeka. Nilisema pia kwamba kuna kiasi cha watu 80 waliojeruhiwa, 60 kati yao wakiwa ni wachimba madini." Alisema Waziri Yiildiz akiwa nje ya mgodi huo.
Vifo hivyo vimesababishwa na hewa ya sumu inayotokana na moto. Hadi asubuhi ya leo, bado moto huo unaosemekana kusababishwa na hitilafu za umeme, ulikuwa ukiendelea kuwaka, masaa 18 baada ya mripuko kutokea.
Juhudi za uokoaji zatatizwa
Waziri Yiildiz pia amesema kuwa baadhi ya wafanyakazi wako umbali wa kilomita mbili chini ya ardhi na usawa wa kilomita nne kutoka lango kuu la kutokea, jambo linalokwamisha jitihada za uokozi. Waandishi wa habari wanasema wachimba madini hao hawakuweza kutumia lifti kujiokoa kwani mripuko huo ulikuwa umekata kabisa umeme mgodini humo.
Waziri Mkuu Tayyip Erdogan ameahirisha ziara yake ya kikazi nje ya nchi na anatazamiwa kulitembelea eneo hilo la ajali, lililo umbali wa kilomita 250 kusini mwa mji mkuu Istanbul.
Kampuni ya Soma Holding inayomiliki mgodi huo imesema mgodi wao ulifanyiwa majaribio ya usalama miezi miwili iliyopita, lakini vyombo vya habari nchini Uturuki vimeripoti kwamba chama tawala cha AKP kilikataa wito wa upinzani bungeni, kutaka mgodi wa Soma kuhakikiwa mwezi uliopita.
Uturuki ina historia ya ajali mbaya za migodini, inayochangiwa na kanuni mbaya za usalama. Mwaka 1992, ajali kama hiyo iliua zaidi ya watu 260 katika mgodi ulio karibu na Bahari Nyeusi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Josephat Charo