1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 130 mbaroni Zambia

16 Agosti 2016

Polisi nchini Zambia imewakamata watu 133 waliokuwa wakiandamana kupinga kuchaguliwa tena kwa Rais Edgar Lungu baada ya mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema kusema kwamba uchaguzi huo ulikuwa wa udangayifu.

https://p.dw.com/p/1JizI
Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Lungu hapo Jumatatu ameshinda uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali kuendelea kuliongoza taifa hilo lenye kushika nafasi ya pili kwa kuzalisha madini ya shaba kwa wingi barani Afrika na ambalo limekuwa likikabiliwa na kudorora kwa uchumi wake kutokana na kuporomoka kwa bei ya bidhaa hiyo.

Mkuu wa polisi wa jimbo la kusini mwa Zambia Godwin Phiri ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba waandamanaji hao walikuwa wakiwalenga wafuasi wa chama tawala kwa kuharibu mali zao.

Ameongeza kusema ni kama vile hujuma zao hizo zimeandaliwa vyema na kwamba walikuwa tu wakisubiri kutangazwa kwa mshindi. Hata hivyo hivi sasa utulivu umerudi nchini humo, amesema Piri.

Zambia ni mojawapo ya nchi za Afrika zenye demokrasia imara licha ya kwamba kulikuwa na vurugu wakati wa kampeni za uchaguzi.Sarafu ya nchi hiyo Kwacha leo imeimarika kwa asilimia 2.5 katika ishara kwamba wawekezaji wamepokea vyema matokeo ya kupatikana kwa mshindi wa moja kwa moja katika uchaguzi huo.

Lungu alishinda kwa asilimia 50.35 dhidi ya asilimia 47.63 alizojipatia Hichilema. Ingelikuwa mgombea amepata ushindi wa chini ya asilimia 50 ingelibidi uchaguzi huo urudiwe

Matokeo yachakachuliwa

Chama cha Hichilema cha Muungano wa Maendeleo ya Taifa (UNPD) kimesema kitapinga matokeo hayo katika mahakama ya Katiba kikiwashutumu maafisa wa uchaguzi kwa udanganyifu wakati wa zoezi la kuhesabu kura ambalo lilianza baada ya kumalizika kwa uchaguzi hapo Alhamisi.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Hakainde Hichilema (UNPD).
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Hakainde Hichilema (UNPD).Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Hichilema amesema "Tunataka uchaguzi huru wa haki na ulio wazi,uchaguzi unaoaminika.Hicho ndicho wanachokita Wazambia. Hawautaki uongozi duni unaotolewa chini ya misingi ya hila kwa kuchakachuwa matokeo."

Kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha UNPD Hichilema amesema katika taarifa hapo jana usiku kwamba chama tawala cha Patriotic Front (PF) kimefanya mapinduzi katika mchakato wa demokrasia nchini Zambia.

Matokeo yashangaza

Rais Edgar Lungu wa Zambia aliyefanikiwa kutetea wadhifa wake.
Rais Edgar Lungu wa Zambia aliyefanikiwa kutetea wadhifa wake.Picha: picture-alliance/dpa/X.Penglijun

Matokeo hayo ya uchaguzi yamewashangaza baadhi ya wachambuzi.Oliver Saasa mchambuzi wa kisiasa na kiuchumi nchini humo amesema kwa kuzingatia hali ya uchumi ya hivi sasa nchini humo asingelitegemea Lungu kushinda kutokana na kwamba ameshindwa kufanya vizuri katika nyanja ya utawala bora na kurudisha imani kwa uchumi.

Marekani imempongeza Lungu kwa ushindi wake huo na kutowa wito kwa wagombea wote kuonyesha uongozi na kuheshimu matokeo rasmi pamoja na kuutaka umma kutumia sheria kushughulikia malalamiko yao.

Serikali ya Marekani pia imezingatia wasi wasi wa waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa juu ya kuongezeka kwa matumizi ya nguvu na vikwazo kwa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kukusanyika mambo ambayo yalijitokeza katika kipindi cha kuelekea uchaguzi huo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Elizabeth Trudeau amesema wanataraji serikali itatilia maanani mashaka hayo kwa ajili ya chaguzi za usoni ili kuimarisha demokrasia nchini Zambia.

Lungu amekuwa madarakani kwa miezi 19 baada ya kushika madaraka kufuatia uchaguzi wa ghafla ulioitishwa baada ya kufariki wakati akiwa madarakani mtangulizi wake Michael Sata.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Daniel Gakuba