Zambia yahalalisha usafirishaji wa bangi kukuza uchumi
17 Desemba 2019Zambia imehalalisha uzalishaji na usafirishaji wa bangi kwa matumizi ya kiafya na kiuchumi. Tangazo hilo limetolewa siku ya Jumatatu na msemaji mkuu wa serikali ya nchi hiyo Dora Siliya baada ya makubaliano ya mkutano maalumu wa baraza la mawaziri.
Zambia inakuwa moja kati ya nchi ambazo hivi karibuni zimebadili msimamo wake juu ya bangi, ili kukuza uchumi wake. Nchi hiyo imehamasika kufanya hivyo kutokana na upungufu wa fedha na deni linaloendelea kukua.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2018 deni la nje la Zambia lilikuwa limefikia dola za kimarekani bilioni 10.5 kutoka bilioni 8.74.
Kiongozi wa Chama cha upinzani cha kijani Peter Sinkamba, ambaye amekuwa akihamasisha uuzwaji wa bangi tangu mwaka 2013, amesema hatua hiyo inaweza kuiingizia Zambia kiasi cha Dola bilioni 36 kwa mwaka.