Zambia yanusurika;Ooh La-laah Bukina Faso
26 Januari 2013Yalitokea pia mabishano makali kuhusu adhabu ya penalti, kadi nyekundu ilitolewa na penalti kuwekwa wavuni na mlinda mlango.
Michezo miwili ya kundi C katika uwanja wa Nelspruit, ikiangaliwa na kundi kubwa kabisa la mashabiki kuweza kuonekana katika wiki ya kwanza ya michuano hiyo, ilifunguliwa na pambano kati ya mabingwa watetezi Zambia dhidi ya Nigeria.
Emmanuel Emenike wa Nigeria aliandika bao kwa vigogo hao wa soka la Afrika baada ya John Obi Mikel kushindwa kuweka wavuni mkwaju wake wa penalti katika kipindi cha kwanza.
Mweene awa shujaa
Lakini gumzo lilizuka pale Zambia ilipozawadiwa penalti ambayo ilionekana kuwa ni ya shaka shaka. Mlinda mlango wa Zambia Kennedy Mweene alikimbia toka langoni mwake na kwenda kuuweka wavuni mpira huo na kuandika bao la kusawazisha kwa timu yake, na kujipatia umaarufu wa kuwa mbabe wa kulinda lango na pia kupachika mabao ya penalti.
Mweene mara nyingi huwa mpigaji wa penalti katika timu yake ya Free State Stars , ya Afrika kusini , na alipachika bao katika mpambano uliomalizika kwa penalti ya ushindi kwa Zambia katika fainali za mwaka jana za kombe la mataifa ya Afrika , dhidi ya Cote D'Ivoire.
Pia ni bingwa wa kuzuwia mikwaju ya penalti, kama alivyothibitisha wakati alipomkatalia Gervihno mwaka jana na tena siku ya Jumatatu pale alipomzuwia Salahadin Said wa Ethiopia kukwamisha mpira wa penalti wavuni.
Nahodha wa Nigeria ambaye pia ndie mlinda mlango wa timu hiyo Vincent Enyeama amekasirishwa mno na uamuzi wa fera kutoka Misri Grisha Ghead. Ni uamuzi mbaya kabisa niliowahi kuona katika historia ya soka, amesema Enyeama.
Baada ya sare hiyo Burkina Faso ilikabiliana na Ethiopia katika uwanja ambao nahodha wa timu ya taifa ya Zambia , Chipolopolo, Christopher Katongo ameuelezea kuwa uwanja mbaya kabisa katika Afrika kusini:
Ethiopia ilianza kwa kishindo, lakini mara tu Burkina Faso ilipoweka mguu vizuri hakuna kilichoweza kuwazuwia wakati Alain Traore alipochangia mabao mawili katika kipigo cha mabo 4-0 dhidi ya Ethiopia.
Ushindi huo ulikuwa mtamu zaidi ukitilia maanani kuwa Burkina Faso ilicheza na watu kumi uwanjani wakati mlinda mlango Abdoulaye Soulama alipoonyeshwa kadi nyekundu.
Leo ni zamu ya Tembo wa Cote D'Ivoire wakitunisha misuli dhidi ya Tunisia na Algeria ina miadi na Togo.
Bundesliga mchezo wa 19
Katika Bundesliga mchezo wa 19 ulianza jana wakati mabingwa watetezi Borussia Dortmund iliiadhibu Nuremberg kwa kuichapa mabao 3-0 nyumbani.
Michezo hiyo inaendelea leo jioni ambapo Borussia Moenchengladbach inaumana na Fortuna Dusseldorf, Eintracht Frankfurt inaikaribisha Hoffenheim, FC Augsburg ina miadi na Schalke 04, Mainz inasafiri kwenda kukumbana na Sport Verreinnigung Greuther Fuerth na Freiburg ni wenyeji wa Bayer Leverkusen. Hapo kesho, Bayern Munich inayoongoza ligi hiyo inatiana kifuani na Stuttgart, na Hamburg Sport Verein iko nyumbani kuikaribisha Werder Bremen.
Mwandishi ; Sekione Kitojo /afpe