Zambia yashindwa kulipia deni lake
18 Novemba 2020Zambia ingeweza kulipa sehemu ya mojawapo ya mikopo ya hati fungani ya dola Ijumaa iliyopita, lakini ikaamua kutofanya hivyo kutokana na haja ya kuwatendea sawa wakopeshaji wake wote, alisema gavana wa benki kuu siku ya Jumatano.
Hata hivyo, waziri wa fedha baadaye alisema uamuzi huo ulikuwa umeongeza kitisho cha wamiliki wa hati fungani hizo zilizotolewa na serikali kuchukua hatua ya kisheria.
Zambia imekuwa nchi ya kwanza ya Afrika kushindwa kulipia deni lake wakati ulimwengu ukikabiliwa na janga la virusi vya corona, baada ya kushindwa kulipa kiasi cha dola milioni 42.5 tarehe ya mwisho ya kipindi cha msamaha kilichokamilika rasmi Ijumaa iliyopita. Wamiliki wa hati fungani za serikali ya Zambia walikuwa wamelikataa ombi la serikali kuahirisha malipo ya faida hadi mwezi Aprili mwakani.
Ikikabiliwa na athari za janga la corona na uchumi unaochechemea, gavana Christopher Mvunga alisema Zambia ilijikuta inatafuta msaada mpana wa kusamehewa deni lake, ikiwa ni pamoja na mfumo wa usitishaji wa kulipia deni unaoungwa mkono na kundi la mataifa tajiri duniani ya 20.
"Mojawapo ya masharti ni kwamba wakopeshaji wote wanatakiwa watendewe sawa...Sio kwamba hatukuweza kulipa. Ni kwamba tukimlipa mkopeshaji mmoja basi tunahitaji kuwalipa wote," Mvunga aliuambia mkutano wa waandishi habari.
Wamiliki wa hati fungani walalamika
Wamiliki wa hatifungani wameikosoa serikali wakisema hatua yake ya kutowajibika imefuta kabisa uwezekano wa kufutiwa deni. Kundi moja la wakopeshaji lilisema huenda likatafakari njia nyingine baada ya Zambia kushindwa kulipa, na hivyo kufungua mlango kwa mchakato wa kuubadili kabisa utaratibu mgumu wa ulipaji deni.
Katika hotuba yake kwa bunge, waziri wa fedha, Bwalya Ng'andu, alisema kushindwa kulipa kiwango cha fedha kilichotakiwa kulisaidia kuboresha mazingira ya kufanya mashauriano na wakopeshaji wengine ambao awali hawakuwa wameonesha nia ya kufanya hivyo.
Hata hivyo, huku akisisitiza kujitolea kwa dhati kwa Zambia kushirikiana kwa uwazi na wakopeshaji katika kutafuta suluhisho, alikiri uamuzi huo ulikuja na athari. "Hizi zinajumuisha wamiliki wa hatifungani kuchukua hatua za kisheria kudai haki zao chini ya makubaliano ya kifedha yaliyopo," alisema na kuongeza kuwa serikali ingeshirikiana kwa karibu na washauri wa kisheria kukabiliana na matokeo yatakayojitokeza.
Uaminifu
Ng'andu alisema serikali inafanya mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, kuhusu nyenzo muafa ya kisera itakayoisaidia kusimamia vyema deni la taifa. Kuhushishwa kwa shirika hilo ni muhimu kuupa uamunifu na nguvu mpya mchakato muafaka wa mabadiliko.
Hatifungani ya mikopo mitatu ilizoshindwa kuzilipia Zambia zinauzwa kwa senti 43 za dola, kwa mujiu wa data za mtandao wa biashara wa kielektroniki, Tradeweb.
Benki kuu ya Zambia pia haikukibadilisha kiwango cha riba ya mikopo, ikikiacha katika asilimia 8.0 siku ya Jumatano.
Mfumuko wa bei, ambao ulipanda hadi asilimia 16 mwezi Oktoba kutoka asilimia 15.7 mwezi Septemba, unatarajiwa kufikia wastani wa asilimia 16.7 katika robo ya nne ya mwaka kabla kushuka hadi kufikia asilimia 13.5 mwaka ujao.
(afp)