1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaporizhhzhia: Ukraine na Urusi zatupiana lawama

Saleh Mwanamilongo
8 Agosti 2022

Ukraine imesema vikosi vya Urusi vinalenga kukata umeme kwenye eneo la kusini mwa nchi hiyo kufuatia shambulio la kombora kwenye kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia.

https://p.dw.com/p/4FH18
Ukraine I Zaporizhzhia I Saporischschja
Picha: Dmytro Smolyenko/Ukrinform/IMAGO

Ukraine imeonya kuhusu hatari ya shambulio la Zaporizhhzhia na kutaka mji huo kutangazwa eneo lisilo na jeshi. Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa wito kwa wakaguzi wa nyuklia wa umoja huo kupewa idhini ya ufikiaji wa mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia, wakati Urusi na Ukraine zikitupiana lawama kufuatia mashambulizi ya mtambo huo.

Katibu Mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres alisema leo kuwa shambulio lolote la mtambo wa nyuklia ni jambo la kujiua.

Petro Kotin, mkuu wa kampuni ya nishati ya nyuklia ya Ukraine ,Energoatom, alitoa wito wa kupelekwa kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa ilikuhifadhi mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia, ambao bado unaendeshwa na mafundi wa Ukraine. Naye balozi wa Ukraine kwenye shirika la umoja wa mataifa la nishati ya nyuklia IAEA ,Yevhenii Tsymbaliuk, aliishutumu Urusi kwa kujaribu kusababisha kukatika kwa umeme kwa kuulenga mtambo wa Zaporizhzhia. Alitoa wito kwa umoja wa mataifa kutuma wachnguzi wake ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

''Serikali ya Zelensky ilifanya kitendo kipya cha ugaidi''

Ukraine imeonya kuhusu hatari ya shambulio la kinu cha nyuklia cha Zaporizhhzhia
Ukraine imeonya kuhusu hatari ya shambulio la kinu cha nyuklia cha Zaporizhhzhia Picha: AP/picture alliance

Shirika la habari la RIA lilimnukuu balozi wa Moscow kwenye shirika la IAEA akisema Urusi iko tayari kuwezesha ziara ya wachunguzi wa IAEA kwenye eneo la kinu hicho. Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi amesema mashambulizi ya Ukraine yameharibu njia za umeme zinazohudumia mtambo huo wa enzi ya KiSovieti,na kusababisha vinu ninne miongoni mwa sita kusitisha huduma zake.

"Mnamo Agosti 7, serikali ya Zelensky ilifanya kitendo kipya cha ugaidi wa nyuklia kwenye miundombinu ya nishati ya Zaporozhzhia ili kusababisha maafa ya kibinadamu katika mikoa ya Kherson na Zaporizhzhia.'' alisema Konashenkov. 

Meli 12 zaondoka Ukraine

Kwingineko, mpango wa kuzuia usafirishaji wa chakula wa Ukraine na urahisishaji uhaba wa kimataifa uliongezeka kwa kasi huku meli mbili za nafaka zikiondoka Bandari za Ukraine za Bahari Nyeusi na kufikia jumla ya 12 tangu meli ya kwanza kusafiri wiki moja iliyopita. Meli mbili za hivi punde zilizosafiri kuelekea Italy na Uturuki zilikuwa zimebeba karibu tani 59,000 tani za mahindi na soya.

Wakati huohuo , chama tawala cha Social Democrat hapa nchini Ujerumani kimesema Kansela wa zamani wa Gerhard Schroeder atasalia kuwa mwanachama wa SPD, baada ya kukuta uhusiano wake na Vladimir Putin kutokiuka sheria za chama hicho.