Zelenskiy azuru Uingereza, apata ahadi ya silaha zaidi
15 Mei 2023Ofisi ya Sunak imesema kiongozi huyo wa Uingereza atathibitisha hii leo utoaji wa mamia ya makombora ya ulinzi wa angani na mifumo mingine ya angani inayojiemndesha yenyewe, ikiwa ni pamoja na mamia ya droni zenye uwezo wa kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 200.
Wiki iliyopita Uingereza ilikuwa nchi ya kwanza kuanza kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu, ambayo yataruhusu vikosi vyake kushambulia vikosi vya Urusi na vituo vya vyake vya ugavi ndani kabisaa ya mstari wa mapambano.
Serikali ya Uingereza imesema Zelenskiy alikuwa tayari amewasili nchini humo na atakutana na Sunak katika makazi yake ya mapumziko.
Soma pia: Zelenskiy asema Urusi itashindwa ndani ya mwaka huu
Sunak amesema katika taarifa kwamba huu ni wakati muhimu katika upinzani wa Ukraine dhidi ya kile alichokiita vita vya kutisha, na kuongeza kuwa taifa hilo linahitaji msaada endelevu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kujilinda dhidi ya mashambulizi yasiokoma na ambayo yamegeuka uhalisia wa kila siku kwa zaidi ya mwaka.
Ofisi ya waziri mkuu imesema Sunak pia atawashinikiza washirika kuipatia Ukraine msaada wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa mataifa ya kundi la G7 nchini Japan baadae wiki hii.
Wakati Zelenskiy akizuru miji mikuu ya Ulaya, Urusi ilizidisha mashambulizi kote Ukraine kwa kutumia droni na makombora mwishoni mwa wiki.
Siku ya Jumapili, Urusi ilizishambulia kwa makombora jamii mbili katika mkoa wa mpakani wa kaskazini wa Sumy, utawala wa kijeshi wa eneo hilo ulisema katika taarifa kwenye chaneli yake rasmi ya Telegram, na kuongeza kuwa milipuko 109 ilirekodiwa.
Ujerumani yaahidi euro bilioni 2.7
Zelenskiy na Macron walikutana na takribani masaa manne katika ikulu ya Elysee jana Jumapili ambapo ofisi ya Macron ilisema Ufaransa itaipatia Ukraine vifaru vyepesi na magari ya kivita katika wiki zijazo, bila kutaja kutaja idadi, lakini pia aliahidi mifumo zaidi ya ulinzi wa anga bila kutoa ufafanuzi.
Soma pia: Rais wa Ukraine azungumza na mwenzake wa China
Ofisi ya Macron ilisema Ufaransa itatoa mafunzo kwa wanajeshi wapatao 2000 wa Ukraine nchini Ufaransa mwaka huu na karibu wengine 4,000 nchini Poland kama sehemu ya juhudi pana za Ulaya.
Ufaransa ilituma ndege kumchukua Zelenskiy nchini Ujerumani, ambako alikutana na Kansela Olaf Scholz mapema hiyo jana na kujadili mipango ya nchi yake ya mashambulizi ya kujibu.
Ilikuwa ziara yake ya kwanza mjini Berlin tangu kuanza kwa uvamizi na ilikuja siku moja baada ya serikali ya Ujerumani kutangaza mpango mpya wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine wenye thamani ya euro bilioni 2.7, ukihusisha vifaru, mifumo ya kudungua ndege na risasi.
Katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Aachen, Zelenskiy pia alipokea tuzo ya kimataifa ya heshima ya Charlamagne, iliyotolewa kwake na watu wa Ukraine. Siku ya Jumamosi, alikutana na papa Francis na waziri Mkuu wa Italia Giorgina Meloni mjini Rome.
Katika ziara yake hiyo ya Ulaya, Zelenskiy amesema Ukraine italenga kukomboa maeneo yanayokaliwa na Urusi ndani ya mipaka ya Ukraine inayotambuliwa kimataifa, na siyo kushambulia ardhi ya Urusi.
Chanzo: Mashirika