Zelensky aitaka Ujerumani kuuvunja ukuta wa Urusi
17 Machi 2022Wito huo ameutoa leo wakati akilihutubia kwa hisia Bunge la Ujerumani kwa njia ya vidio. Zelensky amewaambia wabunge kwamba huo sio ''Ukuta wa Berlin'', ni Ukuta katikati ya Ulaya baina ya uhuru na utumwa na ukuta huo unakuwa mkubwa kutokana na mashambulizi ya mabomu ya kila siku yanayodondoshwa Ukraine.
Zelensky amemtaka Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, kuuvunja Ukuta huo, akikumbushia ombi la Rais wa zamani wa Marekani Ronald Regan alilolitoa kwa Mikhail Gorbachev la kuvunjwa kwa Ukuta wa Berlin wakati wa Vita Baridi.
Pia ameitolea wito Ujerumani kuunga mkono juhudi za Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Aidha, Zelensky ameikosoa Ujerumani kwa kuchelewa kuufuta mradi wenye utata wa bomba la gesi unaogharamiwa na Urusi na Ujerumani unaojulikana kama Nord Stream 2.