Zelensky asema kutotabirika kwa Trump kunaweza kumaliza vita
3 Januari 2025Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema katika mahojiano yaliyorushwa jana kwamba "kutotabirika" kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump kunaweza kusaidia kumaliza vita na Urusi.
Trump, ambaye anatarajiwa kuapishwa rasmi Januari 20, aliahidi kuumaliza mzozo huo uliodumu kwa takriban miaka mitatu ndani ya saa 24 mara tu baada ya kuingia madarakani. Lakini Ukraine imekuwa ikihofia kwamba italazimika kuachia maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi kwa ajili ya upatikanaji wa amani.
Katika mahojiano yake na televisheni ya Ukraine, Zelensky alisema kuwa Trump ana nguvu sana na hatabiriki, na anatamani kuona ushawishi wake ukitumika kwa Urusi.
Kiongozi huyo wa Ukraine amejaribu kuunda uhusiano na timu ya Trump tangu uchaguzi wa Novemba huku kukiwa na hofu kwamba chama cha Republican kinaweza kupunguza msaada muhimu wa kijeshi wa Marekaniau kuusimamisha kabisa.