Zelensky awahimiza washirika kuongeza shinikizo kwa Urusi
28 Mei 2024Aliyasema hayo wakati wa ziara yake jana mjini Madrid, Uhispania, ambayo iliahidi dola bilioni moja katika msaada wa kijeshi huku mashambulizi ya Urusi yakiendelea kushika kasi. Zelensky hata hivyo anasema vikosi vyake vinaendelea kupambana dhidi ya adui katika uwanja wa mapambano.
Urusi imesema imekamata vijiji viwili zaidi kama sehemu ya operesheni yake mashariki mwa Ukraine. Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO - Jens Stoltenberg amewahimiza washirika kutafakari upya vikwazo vyao dhidi ya kutumiwa kwa silaha za Magharibi kufanya mashambulizi ndani ya Urusi, ambalo ni sharti muhimu la rais wa Ukraine.
Marekani na washirika wengine wamekuwa wakisita kuiruhusu Kyiv kushambulia ndani ya Urusi kwa kuhofia kuwa hatua hiyo inaweza kuwaingiza moja kwa moja katika mgogoro na Urusi ambayo ina zana za nyuklia.
Lakini Rais wa Ukraine alisisitiza kuwa lazima washirika wote washirikiane kuiwekea shinikizo sio tu Urusi, bali pia washirika wao ili kuipa Ukraine fursa ya kujilinda yenyewe dhidi ya Urusi. Zelensky anatarajiwa kuwasili leo Brussels kusaini muafaka wa usalama na Ubelgiji na pia anatarajiwa kwenda Ureno.