1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan anatarajia kuimarisha uhusiano na Ujerumani

28 Septemba 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anaendelea na ziara nchini Ujerumani na masuala anayoyapa kipaumbele ni kurudisha uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili na ombi la Uturuki kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/35bmO
Deutschland Recep Tayyip Erdogan, Präsident Türkei | Schloss Bellevue
Picha: Reuters/F. Bensch

Rais Erdogan anaendelea na ziara yake yenye utata na leo ikiwa ni siku ya pili atakuwa na mikutano miwili na Kansela Angela Merkel pamoja na kuzungumza na wandishi habari. Pia atalakiwa rasmi kwa heshima na gwaride la kijeshi katika Ikulu ya Rais ya Bellevue Palace, ambapo atakuwa mgeni wa heshima wa Rais Frank-Walter Steinmeier katika karamu ya kitaifa jioni ya leo.

Uhusiano kuimarika

Ziara hiyo ya siku tatu inatarajiwa kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Kabla ya kuwasili mjini Berlin, Erdogan alitoa wito kwa Uturuki na Ujerumani kufungua ukurasa mpya wa uhusiano kati yao, licha ya kuendelea kwa mvutano uliopo juu ya rekodi ya Uturuki kuhusu haki za binaadamu na masuala mengine.

Ingawa Erdogan ameshazuru Ujerumani mara kadhaa, hii ni ziara ya kwanza ya kitaifa inayoambatana na heshima ya kijeshi. Hata hivyo, Rais Steinmeier amesema ziara hiyo haimaanishi kwamba nchi hizo mbili zitarejea katika uhusiano wake wa kawaida. Steinmeier amesema hawawezi kukubali shinikizo katika vyombo vya habari, mfumo wa mahakama pamoja na vyama vya wafanyakazi.

Deutschland Bundestag
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/H. Hanschke

Kansela Merkel amesema anataka kushirikiana kiuchumi na Uturuki, lakini katika mazungumzo yake na Erdogan atagusia kuhusu masuala muhimu ya haki za binaadamu na wafungwa. Merkel amesema asingependa kuendelea kuiona hali ya haki za binaadamu iliyopo Uturuki na amebainisha kuwa bila shaka watafanikiwa katika makubaliano kadhaa.

Hadi sasa Ujerumani inataka ushahidi zaidi unaoonyesha kuwa kiongozi wa kidini anayeishi nchini Marekani, Fethullah Gulen alihusika na jaribio la kutaka kumpindua Erdogan, mwaka 2016. Suala la Gulen ni moja kati ya masuala yanayosababisha mvutano kati ya Uturuki na Ujerumani.

Shinikizo dhidi ya Erdogan

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International, limemtaka Merkel kuweka shinikizo kwa Erdogan ili awaachie huru wafungwa wa kisiasa.

Kwa mujibu wa shirika hilo, kuna zaidi ya waandishi habari 150 waliofungwa Uturuki, idadi ambayo ni zaidi ya nchi nyingine yoyote, huku mamia ya mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na mashirika ya habari yakifungwa tangu liliposhindwa jaribio la mapinduzi.

Ama kwa upande mwingine, Merkel amesema Ujerumani iko tayari kuisadia kifedha Uturuki kutokana na nchi hiyo kukumbwa na mzozo wa kiuchumi. Akizungumza jana jioni mjini Augsburg, Merkel amesema inabidi upatikane mkakati mzuri utakaoweza kuifanya Uturuki kubakia imara. Kwa mtazamo wake amesema panatakiwa pawepo na ushirikiano wa kiuchumi, kuliko msaada.

Deutschland Protest gegen den Erdogan Besuch am Flughafen Tegel
Waandishi wasio na mipaka ni miongoni mwa mashirika kadhaa yaliyoitisha maandamano Berlin Picha: Reuters/C. Mang

Erdogan amesema wanatafuta lengo la kuongeza uhusiano wa kibiashara na kiuchumi, kwa ajili ya ustawi na mustakabali wa nchi zote hizo mbili. Amesema wanahitaji kuimarisha maslahi yao ya pamoja na kupunguza matatizo yao. Aidha, Erdogan ameonya dhidi ya kuongezeka kwa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wanaoupinga Uislamu nchini Ujerumani na Ulaya kwa ujumla. Amesema wakati mwingine suala la kupinga Uislamu ni kikwazo kikubwa katika mazungumzo ya Uturuki kujiunga kwenye Umoja wa Ulaya.

Mazungumzo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya yamekwama, ingawa nchi hiyo ilitangazwa rasmi kuwa mteuliwa wa uanachana wa umoja huo tangu mwaka 1999.

Rais Erdogan ameongozana na mawaziri wanne pamoja na mkuu wa idara ya ujasusi, Hakan Fidan. Wanasiasa kutoka vyama vya upinzani vya Ujerumani wametangaza kususia dhifa hiyo ya kitaifa, huku wengi wakirudia kuukosoa utawala wa Erdogan. Merkel pia hatarajiwi kuhudhuria karamu hiyo. Kesho Jumamosi, Erdogan anatarajiwa kuufungua msikiti uliopo mjini Cologne ambao umejengwa na shirika la Kiislamu la Uturuki, DITIB.

Hata hivyo, ziara ya Erdogan imetawaliwa na maandamano nchini Ujerumani kupinga utawala wake wa kimabavu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef