1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Putin aonesha nia kujenga mahusiano na Umoja wa Ulaya

Shisia Wasilwa
5 Juni 2018

Rais wa Urusi Vladimir ameonesha nia yake ya kujenga mahusiano na Umoja wa Ulaya wakati ambapo anaelekea Vienna, Austria siku ya Jumanne. Ziara hiyo ni ya kwanza katika nchi ya Umoja wa Ulaya tangu achaguliwe kuwa rais.

https://p.dw.com/p/2yx9f
Werner Faymann und Wladimir Putin
Picha: picture-alliance/dpa/H. Neubauer

Kwenye mahojiano yaliyorushwa mkesha wa ziara hiyo, Putin alikanusha kuwepo kwa mbinu zozote za Urusi za kuugawa na kuudhoofisha Umoja wa Ulaya kwa kujenga mahusiano na makundi maarufu ya kizalendo barani Ulaya.

Aliliambia shirika la habari la Australia la ORF; kuwa, "Inatulazimu kuimarisha mahusiano yetu na Umoja wa Ulaya." Akitaja kuwa eneo hilo ni mshirika mkuu wa biashara wa Urusi.

Austria na Urusi yana mafungamano ya kibiashara

Kwa kuizuru Austria mwanzoni mwa muhula wake wa nne madarakani, Putin alichagua moja ya mataifa machache ya Ulaya ambayo yanatafuta kudumisha mazungumzo na Urusi, licha ya tofauti za Urusi kujihusisha kwenye mizozo iliyoko Ukraine na Syria.

Kansela wa Austria  Sebastian Kurz
Kansela wa Austria Sebastian KurzPicha: Reuters/L. Nieser

Peter Launksy-Tieffenthal, ni Spika wa serikali ya Austria anasema, 

"Mazungumzo ni muhimu zaidi hasa wakati huu ambapo kuna wasiwasi ulimwenguni kote, na yanaweza kusuluhisha badala ya kuipinga Urusi."

Mbali na ilivyokuwa kwa mataifa mengi ya Ulaya, serikali ya mrengo wa kulia ya Austria haijawatimua mabalozi wa Urusi baada ya kisa cha shambulizi la sumu kwa aliyekuwa jasusi wa zamani wa Urusi, Sergei Skripal na binti yake nchini Uingereza.

Baada ya kuwasili, Putin anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Austria Alexander Van der Bellen pamoja na Kansela Sebastian Kurz.

Chama cha Kurz chataka vikwazo dhidi ya Urusi viondolewe

Kurz ambaye ni kiongozi wa kihifadhina anapigia debe Umoja wa Ulaya kuondoa taratibu vikwazo dhidi ya Urusi iwapo kutatoa ufumbuzi wa kumaliza mzozo ulioko Ukraine.

Chama mshiriki wa Kurz cha Freedom Party (FPOe), nacho pia kinaipigia debe hatua hiyo japo kinataka vikwazo vyote dhidi ya Urusi viondolewe.

Rais Vladmir Putin akiwa Vienna
Rais Vladmir Putin akiwa Vienna Picha: AP

Chama hicho cha FPOe kimefikia makubaliano ya ushirikiano na chama tawala cha Urusi cha United Russia party.

Austria ni moja ya mataifa ambayo yanapinga bajeti kubwa ya Umoja wa Ulaya. Ubelgiji inataka mwafaka kuhusu matumizi ya kati ya mwaka 2021-2027 kabla ya uchaguzi ujao wa mwezi Mei.

Kurz alinukuliwa akiliambia gazeti la Ujerumani la Die Welt kuwa Ubelgiji inastahili kuwa mfano mzuri wa kupunguza fedha za matumizi. Anapendekeza kuwa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya inastahili kupunguza wanachama wake kutoka 28 hadi 18 ili kuiimarisha.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, dpa,ap

Mhariri: Grace Patricia Kabogo