Ziara ya waziri mkuu wa India mjini Beijing
15 Januari 2008China na India zinataka kuweka kando tofauti zao na kujishughulisha zaidi siku za mbele na kuimarisaha ushirikiano kati yao.Hicho ndio kiini cha ujumbe wa ziara ya siku kadhaa ya waziri mkuu wa India Manmohan Singh mjini Beijing.
Wataalam wanaashiria,China na India wanaweza haraka kabisa kuipita Marekani kiuchumi.Mahasimu wawili walioteremka vitani mwaka 1962 ,wamegeuka hivi sasa washirika wa kiuchumi.Hata hivyo hali ya kutoaminiana bado haijatoweka moja kwa moja.Mwishoni mwa ziara yake rasmi ya siku kadhaa mjini Beijing,waziri mkuu wa India Manmohan Singh ameelezea matumaini kuona matatizo yanawekwa kando na kujishughulisha badala yake na kuimarisha uhusiano wa pande mbili.Matumaini hayo yanaungwa mkono pia na serikali ya mjini Beijing.
Mnamo miaka ya hivi karibuni,China na India zimeibuka kua madola makuu ya kiuchumi ulimwenguni.Maendeleo hayo ya kiuchumi ndiyo chanzo cha kujongeleana mataifa hayo.Lakini kivuli cha yaliyotoklea zamani kinafunika ushirikiano wao.Mfano ugonvi wa mpakani ambao mpaka sasa bado haujafumbuliwa-suala hilo la mpaka ndilo lililoziteremsha vitani nchi hizo mbili mnamo mwaka 1962.
Hata hivyo waziri mkuu wa India Manmohan Singh anaamini,matatizo ya zamani yataachwa kando.
"Tunatambua majukumu tulio nayo.Tunabidi tuache kando matatizo na mivutano inayokorofisha uhusiano wetu.Tunatambua majaaliwa ni ya aina moja- tangu kijeografia mpaka kihistoria.China na India zinataka hali thabiti na tulivu pamoja na majirani zao na eneo zima la Asia."
Mzozo wa mpakani ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa pia mjini Beijing wakati wa ziara ya waziri m kuu wa India nchini China.Viongozi wa pande hizi mbili wanakubaliano ufumbuzi wa amani unaweza kupatikana haraka.
Masuala kadhaa ya kisiasa yamejadiliwa pia mjini Beijing viongozi wakishadidia dhamiri za kuimarisha ushirikiano siku za mbele.
Nchi zote mbili zimepania kujifunza kutokana na maarifa ya kila upande na kuzidisha ushirikiano katika sekta ya miundo mbinu,namna ya kung'owa umaskini na pia katika mada zinazohusiana na uhaba wa maji safi ya kunywa,mabadiliko ya hali ya hewa,nishati, na katika juhudi za kuupiga vita ugaidi.
Sekta muhimu zaidi ya ushirikiano inatuwama katika uchumi.Biashara ya pande mbili inagonga dala za kimarekani bilioni 20.Hadi kufikia mwaka 2010 viongozi wa India na China wanadhamiria kuzidisha biashara kati ya nchi zao,mara tatu na kufikia kiwango cha dala bilioni 60 za kimarekani.
Badala ya kushindana nani anaongoza barani Asia,India na China zinataka kwa pamoja kushikilia hatamu za uongozi wa bara hilo.