1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya waziri mkuu wa Uturuki nchini Ugiriki.

14 Mei 2010

Vipi kuimarisha uhusiano na kubana matumizi ya kijeshi ?

https://p.dw.com/p/NNMg
George Papandreou, kulia na waziri-mkuu mwenzake Recep Tayyip Erdogan (Uturuki).Picha: AP

Mzozo wa madeni ulioikumba Ugiriki unatarajiwa kuwa chombo ya kuboresha uhusiano na adui wake wa muda mrefu-Uturuki waqkati wa ziara ya leo ya waziri mkuu Tayyip Erdogan wa Uturuki,, mjini Athens. Ziara yake hii ya kwanza ya waziri-mkuu wa Uturuki na ya kwanza mjini Athens tangu 2004,inatarajiwa kutoa ishara ya kuanza enzi mpya ya usuhuba mwema kati ya mahasimu hawa jirani wa kale. Katika ziara hii,waziri-mkuu Erdopgan, anafuatana na mawaziri wake 10 na ujumbe mkubwa wa wanabiashara 150.

Wakati wa ziara hii ya waziri-mkuu Erdogan, mapatano kadhaa ya ushirikiano kati ya Ugiriki na Uturuki, yanatarajiwa kutiwa saini .Isitoshe, waziri-mkuu Erdogan na waziri-mkuu George Papandreou wa Ugiriki, watakuwa wenyekiti wa kikao maalumu cha mabaraza yao 2 ya mawaziri -kikao cha kwanza kabisa cha pamoja na cha aina hii kati ya mahasimu hawa wa kale.

Ajenda ya kikao hicho ni siasa za nje ,usafiri,utalii,mila na utamaduni,elimu,nishati na mazingira.Halkadhalika, tangu Athens hata Ankara,ziliafikiana hivi karibuni kuimarisha uhusiano kati ya majeshi yao ili kupunguza hofu za kuzuka ugomvi baina ya nchi zao mbili.

Mahasimu hawa 2 ,wamefikia ukingoni mwa janga la vita mara 3 ,lakini uhusiano wao ulianza kutengenea hatua kwa hatua, tangu kuzuka mtetemeko wa ardhi katika nchi zao mbili hapo 1999 , hali iliopelekea kila mmoja akimhurumia mwenzake na kusmsaidia.

Licha ya kuboreka kwa uhusiano wao, nchi hizi mbili zimekuwa zikivutana kwa muda mrefu kwa ugomvi wa ardhi katika pwani ya Agean -jambo ambalo lilikaribia kuzusha vita 1996 juu ya kisiwa kisichokaliwa.Pia zimekuwa zikivutana juu ya kisiwa cha Cyprus kilichogawanywa -sehemu 1 ya wacyprus wa asili ya kigiriki na nyengine ya wacyprus wa asili ya kituruki.

Ugiriki, sasa ikiwa imezongwa na madeni na imebidi kubana matumizi na kujkaza mkwiji, nchi zote mbili zimeelezea matumaini kuwa, kila uhusiano wao ukizidi kuimarika,ndipo kutaongoza kupunguza mzigo wa gharama za kijeshi na silaha.Ugiriki, inatumia zaidi ya pato lake la Taifa kwa gharama za ulinzi kuliko nchi yoyote nmwanachama wa Umoja wa Ulaya.Na hii, zaidi inatokana na ugomvi wake na jirani yake Uturuki.

Ugiriki imepewa majuzi mkopo wa Euro Bilioni 110 kiinua -mgongo ili kuiwezesha kulipa madeni yake ili nayo lakini ibane matumizi barabara -jambo ambalo limeongoza malalamiko makali nchini.

Ziara ya waziri-mkuu Erdogan,kwahivyo ,imekuja wakati muwafaka."Hii inaonekana kuwa ni hatua ya kwanza kuleta hali bora ya uelewano tangu msingi kuwekwa 2004....Tutapiga hatua kwa hatua na kuona tuwezacho kufanya."- Afisa wa wizara ya nje ya Ugiriki alisema.

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE

Mhariri: Abdul-Rahman