Zimbabwe itajumuishwa tena katika Jumuiya ya Madola?
20 Aprili 2018Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza, Boris Johnson, atakutana na mwenzake wa Zimbabwe, Sibusiso Moyo, na mawaziri wengine kutoka mataifa jirani ya Afrika kwa mazungumzo yanayotarajiwa kujumuisha uwezekano wa Zimbabwe kuruhusiwa tena kujiunga na jumuiya ya madola Commonwealth.
Zimbabwe ilijiondoa kutoka jumuiya hiyo 2003 baada ya rais wa wakati huo Robert Mugabe kukosolewa kwa chaguzi zilizogubikwa na utata na kutwaliwa kwa nguvu mashamba ya wazungu nchini humo. Mazungumzo ya leo yatafanyika kandoni mwa mkutano wa wakuu wa serikali za mataifa wanachama wa jumuiya ya madola unaofanyika jijini London.
Rais wa sasa wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema anataka nchi yake ijiunge tena na jumuiya hiyo yenye jumla ya nchi 53 zilizokuwa himaya ya Uingereza. Wakati haya yakiarifiwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amelazimika kuondoka katika mkutano wa jumuiya ya madolana jijini London kurejea nyumbani kushughulikia maandamano ya machafuko katika mji mkuu wa jimbo la kaskaszini maghabiribi, Mahikeng, ambako wakazi wamekwamisha shughuli za maisha wakilalamika juu ya utoaji mbovu wa huduma msingi.