Zimbabwe kufanya mazungumzo ya hatua za kuepusha mgomo
30 Januari 2019Serikali ya Zimbabwe itafanya mazungumzo ya hatua za mwisho na vyama vya wafanyakazi wa sekta ya umma leo kujaribu kuepusha mgomo wa nchi nzima ambao unaweza kuzusha machafuko zaidi baada ya maandamano yaliyosababisha ghasia mwezi huu.
Lakini chama kikuu cha waalimu kimesema hakitarajii maendeleo yoyote na tayari kinafanya mipango ya mgomo hapo Februari 5. Msemaji wa rais amesema vikosi vya jeshi vitaendelea kubakia mitaani na serikali itafunga mtandao wa internet tena iwapo ghasia zitazuka.
Waalimu na wafanyakazi wengine wa serikali wanadai ongezeko la mishahara na malipo kwa sarafu ya dola ya Marekani kuwasaidia kupambana na ughali wa maisha na mzozo wa kiuchumi ambao umepunguza mzunguko wa fedha, mafuta na madawa.
Makundi ya haki za binadamu yanasema kiasi ya watu 12 waliuwawa mwezi huu baada ya maandamano ya siku tatu kuhusiana na kupanda kwa bei ya mafuta kusababisha maandamano mitaani na ukandamizaji wa vikosi vya majeshi ya usalama. Serikali inasema watu watatu ndio waliofariki.