Zimbabwe: Miezi sita chini ya rais Mnangagwa
25 Mei 2018Kwa Wazimbabwe, mabadiliko yalimaanisha mwisho wa enzi za Mugabe. Mugabe aliondoka na badala yake mtu anayejulikana kama "mamba" aliwasilisha mwelekeo mpya ambao haukuwa wa kujitenga, bali kufungua njia mpya za maendeleo ya nchi na kuiandaa Zimbabwe kwa uchaguzi ujao. Baada ya miaka kadhaa chini ya Mugabe, wengi walimsherehekea Mnangagwa kama shujaa wa Zimbabwe, wakisahau ukweli kwamba aliwahi kuhudumu kama mtu wa karibu wa Mugabe.
Mwanamuziki mkongwe Thomas Mapfumo ambaye aliwahi kuimba nyimbo dhidi ya utawala wa kikoloni, aliiambia DW kwamba panahitajika mabadiliko ya kweli. Mnamo Aprili mwaka huu, mwanamuziki huyo alifanya tamasha lake la kwanza nchini Zimbabwe baada ya miaka kadhaa ya kuwa uhamishoni: "Hawa ni watu waliofanya kazi na Mugabe. Wanapaswa kuonesha mabadiliko. Watu wanahitaji mabadiliko katika nchi. Na mabadiliko tunayozungumzia si tu yale ya vipodozi. mabadiliko ya kweli tunayohitaji ni uhuru wa kuzungumza, uhuru wa kutembea, watu wetu lazima wapate kazi," alisema Mapfumo.
Katika mstari wa mbele wa mapambano ya kisiasa kwa ajili ya mabadiliko, yupo mwanaharakati na mwanasheria, Doug Coltart, ambaye anakiri kwamba ni kweli uwanja wa kisiasa umefunguliwa. Wauguzi na wafanyakazi wa migodini waliruhusiwa kuandamana, wanaharakati wa haki za binadamu nao wakapaza sauti juu ya malalamiko yao katika mikutano ya wazi iliyorushwa moja kwa moja, na hata kundi moja la sanaa likaonesha igizo kumhusu Mugabe na mke wake. Lakini hayo yanaweza kubadilika.
"Ninafikiri uwanja huu wa siasa utafungwa baada ya uchaguzi kama Mnangagwa atashinda kwa udi na uvumba" anasema Coltart. Msemaji wa rais, George Charamba, amekuwa wazi kwamba kwao uchaguzi huu ni nyenzo katika sera ya kigeni. Coltart anaongeza kwamba ni kama wanataka kujihalalisha, wakati serikali haitaki kukubali kwamba iliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi, lakini wanaelewa kwamba jumuiya ya kimataifa inatambua hivyo na bila ya uchaguzi, watakosa uhalali.
Katika kauli zilizotolewa wiki iliyopita ndani ya baraza la mawaziri la Mnangagwa, zinaashiria kwamba rais huyo alikuwa tayari kutumia ukaribu wake na jeshi ili abakie madarakani. Upinzani na makundi ya haki za binadamu pia yamekataa ukaribu wa jeshi kwa tume ya uchaguzi, pamoja na madai ya kusambazwa kwa wanajeshi katika maeneo ya vijijini kote nchini Zimbabwe.
Ahadi moja ambayo Mnangagwa ameitimiza ni kufungua milango ya biashara ya nchi hiyo. Amewakaribisha wanadiplomasia na wawekezaji na kuomba uanachama tena katika Jumuiya ya Madola.
Mwanauchumi wa Zimbabwe, John Robertson, kwa upande mwingine, ana mtazamo chanya juu ya mustakabali wa baadaye wa nchi hiyo. Anasema changamoto zinazoikabili nchi zilijengwa polepole kwenye mfumo wa miaka 38 ya sera za kiuchumi zilizochaguliwa vibaya. Lakini miezi sita baadaye kipi ambacho kingefanyika ili kubadili hali hiyo kama si kufanya marekebisho? Uchaguzi wa Zimbabwe unatarajiwa kufanyika kati ya mwezi Julai na Agosti.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dw
Mhariri: Mohammed Khelef