1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yatatua changamoto za usafiri

12 Februari 2019

Serikali ya Zimbabwe imelazimika kurejesha usafiri wa mabasi ya abiria ambayo nauli zake ni nafuu ili kuwasaidia wananchi ambao wameathiriwa na huduma hiyo kutokana na maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta.

https://p.dw.com/p/3DDmH
Mosambik Bus
Wazimbabwe wakabiliwa na changamoto za usafiri kutokana na maandamanoPicha: DW/B. Jequete

Mjini Harare katika kituo cha mabasi kumeshuhudiwa zoezi la usafiri wa abiria kwa nauli nafuu likisimamiwa na polisi pamoja na wanajeshi. Hatua hii ya serikali ya kupunguza nauli tofauti na wiki kadhaa zilizopita imepokewa vyema na wananchi wanaotoka mjini humo kuelekea katika maeneo mbalimbali ya nje mwa mji huo.

Shylot Sibanda, mmoja wa abiria, anasema wamefurahishwa na uamuzi wa serikali na ni matarajio yao wataendelea na msimamo huo. "Tumefurahishwa na uamuzi wa serikali, ni matarajio yetu wataendelea hivi magari yanayotoa huduma kwa gharama kubwa yadhibitiwe barabarani ili tumudu kununua chakula na kulipa kodi. Tumefurahi."

Inaelezwa kuwa utaratibu wa gharama nafuu za nauli za mabasi umetokana na mpango maalumu wa serikali kuwauzia mafuta kwa bei nafuu wanaotoa huduma za mabasi ya abiria. Pamoja na hayo serikali ya Zimbabwe kwa sasa ipo kwenye mkakati kabambe wa kulifufua shirika lake la usafiri wa umma, ZUPCO, baada ya kusuasua kwa miaka kadhaa kutokana na usimamizi mbovu na kugubikwa na ufisadi.

Waziri wa uchukuzi wa Zimbabwe, Joel Biggie Matiza, amesema wamechukua hatua za haraka na kuhakikisha wanadhibiti fujo na maandamano baada ya ongezeko la nauli za daladala au mabasi madogo almaarufu kombi. Abiria kwa jina Nomatter Nyakurwa alisema, "Tuko huru hakuna hata tatizo, tumepanda kwenye basi na mwenendo wa kulipa dola tatu za kimarekani umefika mwisho, ni kitu cha zamani hicho."

Mandamano ya kushinikiza utawala wa kisheria

Magari hayo yajulikanayo kwa sifa mbaya ya uendeshaji ambao si makini na usiozingatia sheria za barabarani, na bado wanalalamika hawakutendewa haki kuondolewa katika soko la usafiri nchini humo.

Zimbabwe Fuel Protests
Maafisa wa polisi wakiwa barabarani wakati wa maandamano mjini Harare 14.01.2019Picha: picture alliance/AP Photo

Katika hatua nyingine mjini Harare yalishuhudiwa maandamano zaidi ya wanasheria wakishinikiza serikali kuzingatia utawala wa sheria na kuitaka mahakama ya katiba nchini Zimbabwe kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa ipasavyo. Wanasheria hao walionyesha hofu yao kuwa wanajeshi na polisi nchini humo ni kama wako juu ya sheria kutokana na vitendo vyao vya kuzikanyaga haki za binadamu.

Takriban watu kumi na wawili waliuawa nchini Zimbabwe huku wengine zaidi ya mia wakijeruhiwa na risasi wakati wa maandamano ya kupinga ongezeko kubwa la bei ya mafuta ya dizeli na petroli iliyotangazwa na serikali. Dereva wa teksi David Muchada anasema. "Serikali imewafikiria zaidi wenye mabasi lakini ni vyema wakatuona na sisi wenye teksi angalau tukanunua mafuta kwa dola moja na nusu za Marekani ili nauli zetu zibaki kuwa dola moja. Sisi hatuna tofauti na wenye mabasi."

Katika vituo vya mabasi wanajeshi pamoja na polisi walionekana kusimamia na kuyalinda maeneo hayo kuangalia mzunguko wa abiria na mabasi unaendaje. Mitaani pia ulinzi uliimarishwa. Wataalamu wa uchumi nchini humo waliionya serikali kwamba kama watakubaliana na matakwa ya wananchi wake, uchumi unaweza kuanguka na kuchangia kupanda kwa gharama za maisha.

Mwandishi: Zainab Chondo/ AFPE

Mhariri: Josephat Charo